Sunday, January 16, 2011

U pekee duniani

Mpenzi nakusifia, uzuri wa malaika,
Urembo ulozidia, hakika umeumbika,
Nami ninajivunia, kwako wewe nimefika,
U pekee duniani.

Hakika we u mzuri, kwa sifa zenye kujaa,
Kama nyota alfajiri, maishani unang'aa,
Uzuriwo u dhahiri, hakuna anokataa,
U pekee duniani.

Unayo sauti tamu, nyoka kutoka pangoni,
Mejaa mashamshamu, utamu masikioni,
Huniletea wazimu, kusisimuwa moyoni,
U pekee duniani.

Una rangi asilia, yang'ara kama dhahabu,
Rangi iliyotulia, wengine yawapa gubu,
Sichoki kukusifia, wewe ndo wangu muhibu,
U pekee duniani.

Macho kama ya goroli, na mapole kama njiwa,
Sifa wazistahili, kwani umebarikiwa,
Leo nasema ukweli, wanifanya kunogewa,
U pekee duniani.

Mwendo wako wa kuringa, mrembo mwendo mwendole,
Moyo wangu waukonga, waujaza raha tele,
Nipo radhi kukuhonga, sikupate watu wale,
U pekee duniani.

Sifa zako zimezidi, wewe u nambari wani,
Wewe kwangu maridadi, mwingine simtamani,
Nakupa yangu ahadi, daima 'takuthamini,
U pekee duniani.

Wewe wanipa sababu, kufurahia mapenzi,
Wako ustaarabu, hakika nitakuenzi,
Kukutunza ni wajibu, udumu wetu upenzi,
U pekee duniani.

1 comment:

  1. Uhongise we mtani wangu. Huyu wifi jamani aje nasi tumwone na mwaka huu tunataka iwe harusi. Mtani shairi limetulia na ni bonge la ujumbe kwa wifi nadhani ujumbe umefika.

    ReplyDelete