Friday, January 7, 2011

Tanzania Tanzania

Ukitazama ramani, utaona nchi nzuri,
Ilotamba duniani, ilo na watu wazuri,
Nchi yenye uthamani, ilotupa ufahari,
Tanzania Tanzania, ni wapi twaelekea?

Ilitujua dunia, sie nchi ya amani,
Wote wakatusifia, wengi wakatutamani,
Nchi iliyotulia, yenye raia makini,
Tanzania Tanzania, ni wapi twaelekea?

Kote walikopigana, walikimbilia kwetu,
Hatukuhasimiana, tulijaaliwa utu,
Pamoja kila namna, umoja baina yetu,
Tanzania Tanzania, ni wapi twaelekea?

Tukawa wapatanishi, na wakatusikiliza,
Waliokuwa wabishi, mema tukawaeleza,
Hawakutwona wazushi, kwa sifa tulipendeza,
Tanzania Tanzania, ni wapi twaelekea?

Hakukuwa uhasama, sababu ya madaraka,
Tulitumia hekima, hata tukakubalika,
Viongozi walo wema, hatamu waliishika,
Tanzania Tanzania, ni wapi twaelekea?

Hali imebadilika, Tanzania ipo wapi?
Damu inayomwagika, tumejifunzia wapi?
Mabavu yanotumika, yanatupeleka wapi?
Tanzania Tanzania, ni wapi twaelekea?

Tuseme ndiyo tamaa, yao wetu viongozi?
Ukweli waukataa, ila wao wapagazi,
Pakacha lilochakaa, tuseme hawaliwezi?
Tanzania Tanzania, ni wapi twaelekea?

Tunapoimwaga damu, mioyoni tuna nini?
Nani katulisha sumu, atupe na insulini?
Tupone huu wazimu, ulojaa akilini,
Tanzania Tanzania, ni wapi twaelekea?

Myoyo yajisikiaje, haya yanayotokea?
Upeo watwambiaje, njia twayoelekea?
Wengine watuoneje, kipi tutwaelezea?
Tanzania Tanzania, ni wapi twaelekea?

Hatukuzowea vituko, hivi vyao watawala,
Tena haya machafuko, hayakutokea wala,
Kote kule uendako, amani ilitawala,
Tanzania Tanzania, ni wapi twaelekea?

Nalilia Tanzania, amani inapotea,
Walafi wameingia, hawawezi jionea,
Umoja watukimbia, wenyewe wachekelea,
Tanzania Tanzania, ni wapi twaelekea?

Machozi yananitoka, nchi ninaililia,
Maana imechafuka, mabaya yanatukia,
Madaraka madaraka, kwa wenye kung'ang'ania,
Tanzania Tanzania, ni wapi twaelekea?

Wamenogewa kahawa, wanataka na kakao,
Huona nongwa kugawa, waipate na wenzao,
Nchi yakosa usawa, uhuru ndotoni mwao,
Tanzania Tanzania, ni wapi twaelekea?

Tumjibu nini Mungu, kwau wetu upuuzi?
Kuifanya nchi chungu, tuulinde uongozi,
Amani ile ya tangu, kuitunza hatuwezi,
Tanzania Tanzania, ni wapi twaelekea?

Mungu tumjibu nini, nyie ninawauliza,
Bila huruma myoyoni, nchi mwaiangamiza,
Mwaipata raha gani, binadamu kuwaliza?
Tanzania Tanzania, ni wapi twaelekea?

Nchi tuliyoachiwa, sasa tunaichezea,
Wenzetu wamenogewa, utu umewapotea,
Hawana la kuambiwa, vyeo vimewanogea,
Tanzania Tanzania, ni wapi twaelekea?

Muumba tumrudie, kwani tumemkosea,
Ili atusaidie, kubaya twaelekea,
Eeh Mungu utusikie, nchi yatuelemea,
Tanzania Tanzania, siachi kukulilia.

3 comments:

 1. Jana BUNGE LA 112 LA MAREKANI limeanza kwa KUSOMA KATIBA KWA SAUTI.
  Naamini kwa BUNGE LA TANZANIA walitakiwa wasome shairi hili kwa SAUTI BUNGENI.
  Naambiwa ku-read out loud huweka tofauti kubwa saana.
  "Waheshimiwa" wanahitaji kujua watu wanahisi vipi kuhusu nchi yao
  KAZI NJEMA
  Blessings

  ReplyDelete
 2. shairi limetulia na limesema kila kitu kazi nzuri mtani!!Ubarikiwe

  ReplyDelete
 3. Aisee...sikujua hii asali,
  japo nimekuwa mtu wa kusali,
  Hakika nimeona..honngera diwani ya fadhili.

  ReplyDelete