Monday, January 10, 2011

Siogopi kukupenda

Siogopi kukupenda, hata watu wakisema,
Kukukosa ninakonda, mwilini ninayo homa,
Moyo mbio wanienda, nisikwone siku nzima,
Siogopi kukupenda, hata watu wakisema.

Moyo wangu una wewe, tele tele umejaa,
Ningepatwa na kiwewe, kama ungenikataa,
Mapenzi yote nipewe, nipende kila wasaa,
Siogopi kukupenda, hata watu wakisema.

Maneno nishasikia, yapo tokea kitambo,
Kwa wivu wanaumia, kukukosa ee mrembo,
Kwangu umesharidhia, huhitaji tena nyimbo,
Siogopi kukupenda, hata watu wakisema.

Waseme yote mchana, walale hapo usiku,
Mioyo yawanyongona, imejaa dukuduku,
Sisi tunavyopendana, wamebaki zumbukuku,
Siogopi kukupenda, hata watu wakisema.

Raha kwako naipata, hakika nimeridhika,
Kwako hakuna matata, moyo wangu umefika,
Usiku ninakuota, kwako naliwazika,
Siogopi kukupenda, hata watu wakisema.

Upendo uso kipimo, wewe nimekupatia,
Moyo unalo tuwamo, raha naipata pia,
Kwenye moyo wangu umo, raha yangu ya dunia,
Siogopi kukupenda, hata watu wakisema.

Wenye kusema waseme, waseme hadi wachoke,
Roho zao ziwaume, ziwaume wakereke,
Mioyoni ziwachome, wachomeke wakauke,
Siogopi kukupenda, hata watu wakisema.

Wenye wivu uwashike, uwashike uwagande,
Zaidi wahuzunike, wahuzunike wakonde,
Chakula kisiwashuke, wacha mie nikupende,
Siogopi kukupenda, hata watu wakisema.

Ni raha mwangu moyoni, wewe kuwa ndiwe wangu,
Nimezama furahani, rahani chini ya mbingu,
Sisi tumo mapenzini, tuache ya walimwengu,
Siogopi kukupenda, hata watu wakisema.

1 comment:

  1. hakika hili shairi ni kiboko na yote uliyoandika ni kweli kuna watu wanaacha kazi zao na kuchunguza watu wengine na kuanza kusema sema vimaneno. Mtani wala usiogope kabisa endelea kumpenda huyu umpendae. Nimelipenda sana hili shairi.

    ReplyDelete