Saturday, January 29, 2011

Mola naomba hekima

Dunia inayo mambo, mambo yenye kuzidia,
Mambo kujaa vijambo, utaijua dunia,
Bora 'sifate mkumbo, mambo huleta udhia,
Mola naomba hekima, nikabili haya mambo.

Mola naomba hekima, ili niweze tulia,
Nifunze yaliyo mema, na si mtu kumwonea,
Mdomo usije sema, jambo sijafikiria,
Mola naomba hekima, nikabili haya mambo.

Mola naomba busara, iweze nitangulia,
Nisiifanye papara, mambo yanayonijia,
Unepushie hasira, kichwa kipate tulia,
Mola naomba hekima, nikabili haya mambo.

Mola naomba upole, nao uungwana pia,
An'udhipo mtu yule, ngumi sijemrushia,
Bali nitazame mbele, pasi baya kufanyia,
Mola naomba hekima, nikabili haya mambo.

Mola naomba subira, jambo kutopapakia,
Nifanye niwe imara, mwili na akili pia,
Niepushie madhara, niepushie kulia,
Mola naomba hekima, nikabili haya mambo.

Naomba uvumilivu, hata kwenye kuamua,
Yanipayo maumivu, yale wewe wayajua,
Naomba yalo angavu, n'epushe ya kusumbua,
Mola naomba hekima, nikabili haya mambo.

Mola naomba hekima, nikabili haya mambo,
Mola niweke salama, niwashinde wenye tambo,
Mola naomba uzima, furaha ikawe wimbo,
Mola naomba hekima, nikabili haya mambo.

2 comments:

  1. @Mkuu FADHY: Nimelipenda sana SHAIRI hili Mkuu!
    @MUNGU :

    Naomba HEKIMA!

    ReplyDelete