Tuesday, January 18, 2011

Mama

Mama wewe ni zawadi, ya maisha duniani,
Kwao wowote weledi, wewe unayo thamani,
Kwazo zako juhudi, nikaja ulimwenguni,
Mama wewe ni zawadi, kutoka kwake Muumba.

Kwa malezi yako bora, daima huna kifani,
Kwa zako tele busara, na mwongozo maishani,
Mama wewe ni kinara, nuru yangu maishani.
Mama wewe ni zawadi, kutoka kwake Muumba.

Mama faraja yangu, pindi niwapo shidani,
Hunipooza machungu, moyoni iwe amani,
Nakuombea kwa Mungu, heri tupu duniani,
Mama wewe ni zawadi, kutoka kwake Muumba.

Daima hunipa nguvu, ninapodondoka chini,
Nipatapo maumivu, daima huwa pembeni,
Naupata uangavu, uniwekapo salani,
Mama wewe ni zawadi, kutoka kwake Muumba.

Mama u rafiki mwema, mwingine hapatikani,
Wajali pasi kupima, wajali bila rehani,
Mama nakupenda mama, kutoka mwangu moyoni,
Mama wewe ni zawadi, kutoka kwake Muumba.

Hakuna cha kukulipa, wala hakionekani,
Chochote nitachokupa, hakifikii thamani,
Sala naiweka hapa, akubariki Manani,
Mama wewe ni zawadi, kutoka kwake Muumba.

Mola akujaalie, yalo mema duniani,
Baraka akujazie, akujazie pomoni,
Mabaya akwepushie, ukawe mwenye amani,
Mama wewe ni zawadi, kutoka kwake Muumba.


Heri ya siku ya kuzaliwa mama yangu. Mwenyezi Mungu akupe miaka mingi zaidi. Ninakupenda sana.

Nimeandika shairi hili maalumu kwa mama yangu na akina mama wengine wote. Ninyi ni zawadi za thamani zaidi ambazo mwanadamu hupata kuwa nazo. Lazima mjivunie kuwa kina mama kwa kuwa sisi mliotuzaa, tunawapenda sana kwa hakika. Mungu awabariki sana.

5 comments:

  1. Kwanza nasema HONGERA SANA kwa siku ya kuzaliwa mama. shairi lina ujumbe mzuri unasoma mpaka unapatwa na hisia za aina yako. Ahsante Fadhy Mtani. Hakika ni kweli hakuna kama mama kama kuna mtu hajamwambia mama yake ni vipi anampenda basi achukue nafasi na kumwambia. Ni jambo la muhimu sana. HONERA SANA KWA SIKU YA KUZALIWA uwe na siku njema sana.

    ReplyDelete