Thursday, January 13, 2011

Lini utakuwa wangu?

Siupati usingizi, mwenzio nafikiria,
Nipo hoi sijiwezi, wewe tu nakuwazia,
Napenda niwekwe wazi, kwani nazidi umia,
Lini utakuwa wangu, tena wangu peke yangu?

Mawazo yanikondesha, nakonda sijitambui,
Homa unanipandisha, juu yako sijijui,
Jibu walichelewesha, hata mlo sichukui,
Lini utakuwa wangu, tena wangu peke yangu?

Nambie nikusikie, nikusikie jamani,
Niepushe nisilie, niweke mwako moyoni,
Na mie nijisikie, ninapendwa duniani,
Lini utakuwa wangu, tena wangu peke yangu?

Lini utanikubali, ili niache teseka,
Nambie basi ukweli, niache kuweweseka,
Wajua sinayo hali, kwako wewe nimefika,
Lini utakuwa wangu, tena wangu peke yangu?

Lini utanipa jibu, moyo upate tulia,
Ukimya wako adhabu, wanifanya kuumia,
Yaseme yalo irabu, kuwa wanikubalia,
Lini utakuwa wangu, tena wangu peke yangu?

Lini utanikubali, nambie nifurahie,
Wala usiende mbali, juu yangu jisikie,
Upendo ulo aghali, penzi nikuhifadhie,
Lini utakuwa wangu, tena wangu peke yangu?

Usikubali kwingine, peke yangu nakufaa,
Njoo kwangu tupendane, mapenzi yenye kung'aa,
Tupendane tufaane, moyoni umenijaa,
Lini utakuwa wangu, tena wangu peke yangu?

3 comments:

 1. Fadhy Mtani usikata tamaa mtskuja kuwa pamoja nina imani. Natumaini huyo unayemlilia anakusikia. Na nina imani kama kweli anajua kwa kweli si muda mrefu atasikia tu kilio chaku na mtalifaidi tu hilo penzi. Mtani nakitakia kila la kheri mtani wifi umpata karibuni kwani inaonekana unampenda kweli na unamwitaji mno. Shairi bombi kwelikweli. Hongera kwa kipaji hiki.Binafsi nimelipenda mno hata kama lina mlengwa. Upendo daima.

  ReplyDelete
 2. Fadhy,
  Shairi zuri sana hili.Vina vimekaa mahali pake na ujumbe ni murua kabisa.

  Kama alivyosema Da Yasinta hapo juu,kama ni kweli kuna ambaye moyo wako unamlilia,basi yu mbioni.Subra huvuta kheri.Na kama umeliandika kwa ujumla,basi kwingineko kwenye mapenzi na bashasha napo subra ndio muhimu.Kazi nzuri

  ReplyDelete
 3. Kama kweli siyo usanii, huyo mpenzi wako lazima awe wa peke yako. Imetulia.

  ReplyDelete