Saturday, January 29, 2011

Mola naomba hekima

Dunia inayo mambo, mambo yenye kuzidia,
Mambo kujaa vijambo, utaijua dunia,
Bora 'sifate mkumbo, mambo huleta udhia,
Mola naomba hekima, nikabili haya mambo.

Mola naomba hekima, ili niweze tulia,
Nifunze yaliyo mema, na si mtu kumwonea,
Mdomo usije sema, jambo sijafikiria,
Mola naomba hekima, nikabili haya mambo.

Mola naomba busara, iweze nitangulia,
Nisiifanye papara, mambo yanayonijia,
Unepushie hasira, kichwa kipate tulia,
Mola naomba hekima, nikabili haya mambo.

Mola naomba upole, nao uungwana pia,
An'udhipo mtu yule, ngumi sijemrushia,
Bali nitazame mbele, pasi baya kufanyia,
Mola naomba hekima, nikabili haya mambo.

Mola naomba subira, jambo kutopapakia,
Nifanye niwe imara, mwili na akili pia,
Niepushie madhara, niepushie kulia,
Mola naomba hekima, nikabili haya mambo.

Naomba uvumilivu, hata kwenye kuamua,
Yanipayo maumivu, yale wewe wayajua,
Naomba yalo angavu, n'epushe ya kusumbua,
Mola naomba hekima, nikabili haya mambo.

Mola naomba hekima, nikabili haya mambo,
Mola niweke salama, niwashinde wenye tambo,
Mola naomba uzima, furaha ikawe wimbo,
Mola naomba hekima, nikabili haya mambo.

Tuesday, January 18, 2011

Mama

Mama wewe ni zawadi, ya maisha duniani,
Kwao wowote weledi, wewe unayo thamani,
Kwazo zako juhudi, nikaja ulimwenguni,
Mama wewe ni zawadi, kutoka kwake Muumba.

Kwa malezi yako bora, daima huna kifani,
Kwa zako tele busara, na mwongozo maishani,
Mama wewe ni kinara, nuru yangu maishani.
Mama wewe ni zawadi, kutoka kwake Muumba.

Mama faraja yangu, pindi niwapo shidani,
Hunipooza machungu, moyoni iwe amani,
Nakuombea kwa Mungu, heri tupu duniani,
Mama wewe ni zawadi, kutoka kwake Muumba.

Daima hunipa nguvu, ninapodondoka chini,
Nipatapo maumivu, daima huwa pembeni,
Naupata uangavu, uniwekapo salani,
Mama wewe ni zawadi, kutoka kwake Muumba.

Mama u rafiki mwema, mwingine hapatikani,
Wajali pasi kupima, wajali bila rehani,
Mama nakupenda mama, kutoka mwangu moyoni,
Mama wewe ni zawadi, kutoka kwake Muumba.

Hakuna cha kukulipa, wala hakionekani,
Chochote nitachokupa, hakifikii thamani,
Sala naiweka hapa, akubariki Manani,
Mama wewe ni zawadi, kutoka kwake Muumba.

Mola akujaalie, yalo mema duniani,
Baraka akujazie, akujazie pomoni,
Mabaya akwepushie, ukawe mwenye amani,
Mama wewe ni zawadi, kutoka kwake Muumba.


Heri ya siku ya kuzaliwa mama yangu. Mwenyezi Mungu akupe miaka mingi zaidi. Ninakupenda sana.

Nimeandika shairi hili maalumu kwa mama yangu na akina mama wengine wote. Ninyi ni zawadi za thamani zaidi ambazo mwanadamu hupata kuwa nazo. Lazima mjivunie kuwa kina mama kwa kuwa sisi mliotuzaa, tunawapenda sana kwa hakika. Mungu awabariki sana.

Sunday, January 16, 2011

U pekee duniani

Mpenzi nakusifia, uzuri wa malaika,
Urembo ulozidia, hakika umeumbika,
Nami ninajivunia, kwako wewe nimefika,
U pekee duniani.

Hakika we u mzuri, kwa sifa zenye kujaa,
Kama nyota alfajiri, maishani unang'aa,
Uzuriwo u dhahiri, hakuna anokataa,
U pekee duniani.

Unayo sauti tamu, nyoka kutoka pangoni,
Mejaa mashamshamu, utamu masikioni,
Huniletea wazimu, kusisimuwa moyoni,
U pekee duniani.

Una rangi asilia, yang'ara kama dhahabu,
Rangi iliyotulia, wengine yawapa gubu,
Sichoki kukusifia, wewe ndo wangu muhibu,
U pekee duniani.

Macho kama ya goroli, na mapole kama njiwa,
Sifa wazistahili, kwani umebarikiwa,
Leo nasema ukweli, wanifanya kunogewa,
U pekee duniani.

Mwendo wako wa kuringa, mrembo mwendo mwendole,
Moyo wangu waukonga, waujaza raha tele,
Nipo radhi kukuhonga, sikupate watu wale,
U pekee duniani.

Sifa zako zimezidi, wewe u nambari wani,
Wewe kwangu maridadi, mwingine simtamani,
Nakupa yangu ahadi, daima 'takuthamini,
U pekee duniani.

Wewe wanipa sababu, kufurahia mapenzi,
Wako ustaarabu, hakika nitakuenzi,
Kukutunza ni wajibu, udumu wetu upenzi,
U pekee duniani.

Thursday, January 13, 2011

Lini utakuwa wangu?

Siupati usingizi, mwenzio nafikiria,
Nipo hoi sijiwezi, wewe tu nakuwazia,
Napenda niwekwe wazi, kwani nazidi umia,
Lini utakuwa wangu, tena wangu peke yangu?

Mawazo yanikondesha, nakonda sijitambui,
Homa unanipandisha, juu yako sijijui,
Jibu walichelewesha, hata mlo sichukui,
Lini utakuwa wangu, tena wangu peke yangu?

Nambie nikusikie, nikusikie jamani,
Niepushe nisilie, niweke mwako moyoni,
Na mie nijisikie, ninapendwa duniani,
Lini utakuwa wangu, tena wangu peke yangu?

Lini utanikubali, ili niache teseka,
Nambie basi ukweli, niache kuweweseka,
Wajua sinayo hali, kwako wewe nimefika,
Lini utakuwa wangu, tena wangu peke yangu?

Lini utanipa jibu, moyo upate tulia,
Ukimya wako adhabu, wanifanya kuumia,
Yaseme yalo irabu, kuwa wanikubalia,
Lini utakuwa wangu, tena wangu peke yangu?

Lini utanikubali, nambie nifurahie,
Wala usiende mbali, juu yangu jisikie,
Upendo ulo aghali, penzi nikuhifadhie,
Lini utakuwa wangu, tena wangu peke yangu?

Usikubali kwingine, peke yangu nakufaa,
Njoo kwangu tupendane, mapenzi yenye kung'aa,
Tupendane tufaane, moyoni umenijaa,
Lini utakuwa wangu, tena wangu peke yangu?

Monday, January 10, 2011

Siogopi kukupenda

Siogopi kukupenda, hata watu wakisema,
Kukukosa ninakonda, mwilini ninayo homa,
Moyo mbio wanienda, nisikwone siku nzima,
Siogopi kukupenda, hata watu wakisema.

Moyo wangu una wewe, tele tele umejaa,
Ningepatwa na kiwewe, kama ungenikataa,
Mapenzi yote nipewe, nipende kila wasaa,
Siogopi kukupenda, hata watu wakisema.

Maneno nishasikia, yapo tokea kitambo,
Kwa wivu wanaumia, kukukosa ee mrembo,
Kwangu umesharidhia, huhitaji tena nyimbo,
Siogopi kukupenda, hata watu wakisema.

Waseme yote mchana, walale hapo usiku,
Mioyo yawanyongona, imejaa dukuduku,
Sisi tunavyopendana, wamebaki zumbukuku,
Siogopi kukupenda, hata watu wakisema.

Raha kwako naipata, hakika nimeridhika,
Kwako hakuna matata, moyo wangu umefika,
Usiku ninakuota, kwako naliwazika,
Siogopi kukupenda, hata watu wakisema.

Upendo uso kipimo, wewe nimekupatia,
Moyo unalo tuwamo, raha naipata pia,
Kwenye moyo wangu umo, raha yangu ya dunia,
Siogopi kukupenda, hata watu wakisema.

Wenye kusema waseme, waseme hadi wachoke,
Roho zao ziwaume, ziwaume wakereke,
Mioyoni ziwachome, wachomeke wakauke,
Siogopi kukupenda, hata watu wakisema.

Wenye wivu uwashike, uwashike uwagande,
Zaidi wahuzunike, wahuzunike wakonde,
Chakula kisiwashuke, wacha mie nikupende,
Siogopi kukupenda, hata watu wakisema.

Ni raha mwangu moyoni, wewe kuwa ndiwe wangu,
Nimezama furahani, rahani chini ya mbingu,
Sisi tumo mapenzini, tuache ya walimwengu,
Siogopi kukupenda, hata watu wakisema.

Friday, January 7, 2011

Tanzania Tanzania

Ukitazama ramani, utaona nchi nzuri,
Ilotamba duniani, ilo na watu wazuri,
Nchi yenye uthamani, ilotupa ufahari,
Tanzania Tanzania, ni wapi twaelekea?

Ilitujua dunia, sie nchi ya amani,
Wote wakatusifia, wengi wakatutamani,
Nchi iliyotulia, yenye raia makini,
Tanzania Tanzania, ni wapi twaelekea?

Kote walikopigana, walikimbilia kwetu,
Hatukuhasimiana, tulijaaliwa utu,
Pamoja kila namna, umoja baina yetu,
Tanzania Tanzania, ni wapi twaelekea?

Tukawa wapatanishi, na wakatusikiliza,
Waliokuwa wabishi, mema tukawaeleza,
Hawakutwona wazushi, kwa sifa tulipendeza,
Tanzania Tanzania, ni wapi twaelekea?

Hakukuwa uhasama, sababu ya madaraka,
Tulitumia hekima, hata tukakubalika,
Viongozi walo wema, hatamu waliishika,
Tanzania Tanzania, ni wapi twaelekea?

Hali imebadilika, Tanzania ipo wapi?
Damu inayomwagika, tumejifunzia wapi?
Mabavu yanotumika, yanatupeleka wapi?
Tanzania Tanzania, ni wapi twaelekea?

Tuseme ndiyo tamaa, yao wetu viongozi?
Ukweli waukataa, ila wao wapagazi,
Pakacha lilochakaa, tuseme hawaliwezi?
Tanzania Tanzania, ni wapi twaelekea?

Tunapoimwaga damu, mioyoni tuna nini?
Nani katulisha sumu, atupe na insulini?
Tupone huu wazimu, ulojaa akilini,
Tanzania Tanzania, ni wapi twaelekea?

Myoyo yajisikiaje, haya yanayotokea?
Upeo watwambiaje, njia twayoelekea?
Wengine watuoneje, kipi tutwaelezea?
Tanzania Tanzania, ni wapi twaelekea?

Hatukuzowea vituko, hivi vyao watawala,
Tena haya machafuko, hayakutokea wala,
Kote kule uendako, amani ilitawala,
Tanzania Tanzania, ni wapi twaelekea?

Nalilia Tanzania, amani inapotea,
Walafi wameingia, hawawezi jionea,
Umoja watukimbia, wenyewe wachekelea,
Tanzania Tanzania, ni wapi twaelekea?

Machozi yananitoka, nchi ninaililia,
Maana imechafuka, mabaya yanatukia,
Madaraka madaraka, kwa wenye kung'ang'ania,
Tanzania Tanzania, ni wapi twaelekea?

Wamenogewa kahawa, wanataka na kakao,
Huona nongwa kugawa, waipate na wenzao,
Nchi yakosa usawa, uhuru ndotoni mwao,
Tanzania Tanzania, ni wapi twaelekea?

Tumjibu nini Mungu, kwau wetu upuuzi?
Kuifanya nchi chungu, tuulinde uongozi,
Amani ile ya tangu, kuitunza hatuwezi,
Tanzania Tanzania, ni wapi twaelekea?

Mungu tumjibu nini, nyie ninawauliza,
Bila huruma myoyoni, nchi mwaiangamiza,
Mwaipata raha gani, binadamu kuwaliza?
Tanzania Tanzania, ni wapi twaelekea?

Nchi tuliyoachiwa, sasa tunaichezea,
Wenzetu wamenogewa, utu umewapotea,
Hawana la kuambiwa, vyeo vimewanogea,
Tanzania Tanzania, ni wapi twaelekea?

Muumba tumrudie, kwani tumemkosea,
Ili atusaidie, kubaya twaelekea,
Eeh Mungu utusikie, nchi yatuelemea,
Tanzania Tanzania, siachi kukulilia.