Monday, December 6, 2010

Yupo Wapi?

Bado ninamtafuta, mpenzi aso na doa,
Ni wapi nitamkuta, nami niweze mwopoa,
Ni wapi pa kumpata, sitaki wa kudokoa,
Nani hana hata doa, ni wapi pa kumkuta?

Sitaki mwenye kasoro, ila alokamilika,
Simtaki mwenda doro, kigulu njia kuruka,
Yule awaye mwororo, wa sura isopauka,
Simtaki wa kuzodoa, asiyejua kunata.

Mpenzi alo na sifa, zijae dunia yote,
Aloumbika hajafa, kizani ameremete,
Mjuvi wa maarifa, mwendo mwendole apate,
Watu macho kukodoa, watamani kumpata.

Mpenzi tabia njema, asiwepo mfanowe,
Avume dunia nzima, kote azungumziwe,
Mkamilifu waama, kamwe asitindikiwe,
Tabia yenye kupoa, aso na makuu hata.

Alipo nionesheni, mie ninamhitaji,
Aje nimuweke ndani, kwa penzi anifariji,
Nitambe ulimwenguni, nij’one nina kipaji,
Watu roho kunyongoa, mie jasho anifuta.

Nazunguka duniani, niambieni aliko,
Nipae hata angani, nimfate huko huko,
Nimhonge bilioni, anitoe hamaniko,
Ni lepe lanikong’oa, nawaza pa kumpata.

Wala sitaki zeeka, nizeeke sijamwona,
Nd’o ma’na nahangaika, pengine tutakutana,
Wa sifa za malaika, kifani kiwe hakuna,
Kucha jicho nakodoa, nikilala nitamwota?

Nambieni kama yupo, mpenzi aso kasoro,
Furaha tele iwepo, kusiwe na migogoro,
Uvume vema upepo, kamwe kisiwe kihoro,
Moyo kutoutoboa, bali raha kuipata.

3 comments:

 1. kwanza nanukuu
  "Wala sitaki zeeka, nizeeke sijamwona,
  Nd’o ma’na nahangaika, pengine tutakutana,
  Wa sifa za malaika, kifani kiwe hakuna,
  Kucha jicho nakodoa, nikilala nitamwota?" mwiaho wa kunuuu:- mtani usiwe na wasiwasi wako utanpata tu na atakupa hicho ukitakacho. Mtaishi maisha mazuri na wote mtayafurahia na watoto mtapata. Na wala hutazeeka bila kumwona.

  ReplyDelete
 2. Msijazane ila mfurike,
  sufuria na chungu vyote usifunike.

  ReplyDelete