Thursday, December 30, 2010

Penzi letu la wawili

Majira hubadilika,
Miaka inasogea,
Nyasi nazo hunyauka,
Mimea kujiozea,
Lakini nina hakika,
Wewe hutonipotea.

Wewe unayo thamani,
Ya upendo ulo kweli,
U pekee duniani,
Ambaye wastahili,
Kukupa yalo moyoni,
Kwa pendo letu wawili.

Mi nawe twapendezana,
Kwa pendo lililoshiba,
Hakika tunatoshana,
Kwa dhati pia kwa huba,
Pendo tunalopeana,
Linayo tele mahaba.

Wanipa mie furaha,
U zawadi maishani,
Kuwa nawe kuna raha,
Ni raha iso kifani,
Nafurahi kwa madaha,
Waridi langu moyoni.

3 comments:

  1. Hakika watu wana vipaji,
    Nina uhakika mlengwa anajivuna sana kuandikiwa beti kama hizi maana leo mtani naona hili la kufungia mwaka. Shairi tamu unasoma mpaka machozi sijui wivu nao ni kosa? Kwa kweli jamani Mapenzi matamu. Uhongise mtani kwa kutujumuisha.!!!

    ReplyDelete
  2. Hivi maandishi matamu sio aina moja wapo ya kuloga mtu aka uchawi?

    ReplyDelete