Monday, December 13, 2010

Nakuota nilalapo

Ndotoni unanijia, mapenzi waniletea,
Wanipa kufurahia, furaha kuninogea,
Moyo wangu hutulia, penzini kuogelea,
Nakuota nilalapo.

Ndotoni unanijia, wanipenda wanambia,
Waniambia 'tulia', nami ninakusikia,
Neno unalonambia, moyoni laniingia,
Nakuota nilalapo.

Ndotoni unanijia, mara wanikumbatia,
Moyo kasi wakimbia, raha tele nasikia,
Machoni nakwangalia, kwa furaha unalia,
Nakuota nilalapo.

Ndotoni unanijia, waisogeza hatua,
Busu unanipatia, mwili lausisimua,
Raha tele yanijia, kukukosa 'taugua,
Nakuota nilalapo.

Ndotoni unanijia, na penzi lilokolea,
Mahaba wanipatia, hakika yaninogea,
Raha inanizidia, moyoni nachekelea,
Nakuota nilalapo.

Ndotoni unanijia, mkono wauchukua,
Kisha wewe wanambia, kwangu mimi umetua,
Mbali hutoangalia, kwani umenichagua,
Nakuota nilalapo.

Ndotoni unanijia, siachi kukuwazia,
Hakika nakuzimia, wewe nakufikiria,
Natamani kutukia, kamwe sije nikimbia,
Nakuota nilalapo.

3 comments:

  1. una kipajjjji na utafika mbali

    seriously nimelipendaaaaaaaa

    ReplyDelete
  2. Mlengwa wa shairi hili inabidi afurahie mtani ipo siku hayo ulioandika au unayoyaota yatakuwa kweli nakuombea. Kusema kweli nimelipenda sana shairi hili.

    ReplyDelete