Thursday, December 30, 2010

Penzi letu la wawili

Majira hubadilika,
Miaka inasogea,
Nyasi nazo hunyauka,
Mimea kujiozea,
Lakini nina hakika,
Wewe hutonipotea.

Wewe unayo thamani,
Ya upendo ulo kweli,
U pekee duniani,
Ambaye wastahili,
Kukupa yalo moyoni,
Kwa pendo letu wawili.

Mi nawe twapendezana,
Kwa pendo lililoshiba,
Hakika tunatoshana,
Kwa dhati pia kwa huba,
Pendo tunalopeana,
Linayo tele mahaba.

Wanipa mie furaha,
U zawadi maishani,
Kuwa nawe kuna raha,
Ni raha iso kifani,
Nafurahi kwa madaha,
Waridi langu moyoni.

Monday, December 13, 2010

Nakuota nilalapo

Ndotoni unanijia, mapenzi waniletea,
Wanipa kufurahia, furaha kuninogea,
Moyo wangu hutulia, penzini kuogelea,
Nakuota nilalapo.

Ndotoni unanijia, wanipenda wanambia,
Waniambia 'tulia', nami ninakusikia,
Neno unalonambia, moyoni laniingia,
Nakuota nilalapo.

Ndotoni unanijia, mara wanikumbatia,
Moyo kasi wakimbia, raha tele nasikia,
Machoni nakwangalia, kwa furaha unalia,
Nakuota nilalapo.

Ndotoni unanijia, waisogeza hatua,
Busu unanipatia, mwili lausisimua,
Raha tele yanijia, kukukosa 'taugua,
Nakuota nilalapo.

Ndotoni unanijia, na penzi lilokolea,
Mahaba wanipatia, hakika yaninogea,
Raha inanizidia, moyoni nachekelea,
Nakuota nilalapo.

Ndotoni unanijia, mkono wauchukua,
Kisha wewe wanambia, kwangu mimi umetua,
Mbali hutoangalia, kwani umenichagua,
Nakuota nilalapo.

Ndotoni unanijia, siachi kukuwazia,
Hakika nakuzimia, wewe nakufikiria,
Natamani kutukia, kamwe sije nikimbia,
Nakuota nilalapo.

Monday, December 6, 2010

Yupo Wapi?

Bado ninamtafuta, mpenzi aso na doa,
Ni wapi nitamkuta, nami niweze mwopoa,
Ni wapi pa kumpata, sitaki wa kudokoa,
Nani hana hata doa, ni wapi pa kumkuta?

Sitaki mwenye kasoro, ila alokamilika,
Simtaki mwenda doro, kigulu njia kuruka,
Yule awaye mwororo, wa sura isopauka,
Simtaki wa kuzodoa, asiyejua kunata.

Mpenzi alo na sifa, zijae dunia yote,
Aloumbika hajafa, kizani ameremete,
Mjuvi wa maarifa, mwendo mwendole apate,
Watu macho kukodoa, watamani kumpata.

Mpenzi tabia njema, asiwepo mfanowe,
Avume dunia nzima, kote azungumziwe,
Mkamilifu waama, kamwe asitindikiwe,
Tabia yenye kupoa, aso na makuu hata.

Alipo nionesheni, mie ninamhitaji,
Aje nimuweke ndani, kwa penzi anifariji,
Nitambe ulimwenguni, nij’one nina kipaji,
Watu roho kunyongoa, mie jasho anifuta.

Nazunguka duniani, niambieni aliko,
Nipae hata angani, nimfate huko huko,
Nimhonge bilioni, anitoe hamaniko,
Ni lepe lanikong’oa, nawaza pa kumpata.

Wala sitaki zeeka, nizeeke sijamwona,
Nd’o ma’na nahangaika, pengine tutakutana,
Wa sifa za malaika, kifani kiwe hakuna,
Kucha jicho nakodoa, nikilala nitamwota?

Nambieni kama yupo, mpenzi aso kasoro,
Furaha tele iwepo, kusiwe na migogoro,
Uvume vema upepo, kamwe kisiwe kihoro,
Moyo kutoutoboa, bali raha kuipata.