Saturday, November 27, 2010

Tanesco mnakera

Tanesco mnakera, ukweli leo nasema,
Mnatutia hasira, kwani hamna huruma,
Mnatutia hasara, ni mbovu yenu huduma,
Kata kata ya umeme, Tanesco mnakera.

Hata huruma hakuna, mwaonesha hamjali,
Umeme mwakata sana, hakuna hata kauli,
Nyie hamna maana, daima siyo wakweli,
Kata kata ya umeme, Tanesco mnakera.

Hakuna maisha bora, Tanesco mwazingua,
Biashara zadorora, vitu vyetu vyaungua,
Nasema kweli mwakera, umeme navyosumbua,
Kata kata ya umeme, Tanesco mnakera.

Sisi wenye masaluni, mwataka tukale wapi?
Tanesco mna nini, kwani bili hatulipi?
Mwatupa umasikini, ama wote twuze pipi?
Kata kata ya umeme, Tanesco mnakera.

Sisi tuuzao maji, Tanesco mwatukera,
Umeme ndiyo mtaji, kwenye yetu biashara,
Lakini hamuhitaji, tupate maisha bora,
Kata kata ya umeme, Tanesco mnakera.

Wale wauza barafu, ama wenye mahoteli,
Wapata uharibifu, nyie wala hamjali,
Huo wenu unyamafu, bora mkafie mbali,
Kaka kata ya umeme, Tanesco mnakera.

Kiujumla mwakera, tena mnatuchefua,
Mwaongeza ufukara, hakya kweli mwatibua,
Hiyo yenu mishahara, ni bora ingepungua,
Kata kata ya umeme, Tanesco mnakera.

Tena mwafanya kusudi, taifa mwalikomoa,
Huo wenu ufisadi, siku moja yawajia,
Hakika itatubidi, vitini kuwaondoa,
Kata kata ya umeme, Tanesco mnakera.

Bora itungwe sheria, wengine waruhusiwe,
Umeme kutuletea, Tanesco mkimbiwe,
Wabunge nyote sikia, twaomba tusaidiwe,
Kata kata ya umeme, Tanesco mnakera.

Rais fanya hatua, ulisafishe shirika,
Wananchi twaumia, limeoza linanuka,
Vitu watuunguzia, utu ulishawatoka,
Kata kata ya umeme, Tanesco mnakera.

Ya kusema nimesema, ujumbe umeshafika,
Tanesco siyo wema, hali ishaharibika,
Siku moja mtakoma, kwani tushakasirika.
Kata kata ya umeme, Tanesco mnakera.

1 comment:

  1. napenda watu wasemayo walionayo moyoni na hili shairi ilibidi kabisa raisi alisome kwani ni kweli kero mno kutatiwa umeme. Mtani leo umenena...

    ReplyDelete