Monday, November 15, 2010

Bado nipo

Sikuishika kalamu, siku nyingi zimepita,
Sikuwapeni salamu, hadi moyo wanipwita,
Sasa napata wazimu, kuhisi mshanifuta,
Ndugu yenu bado nipo, msidhani sipo tena.

Sijui ni majukumu, haya yamenikamata,
Uvivu kwangu ni sumu, wala usingenipata,
Nikatingwa mumu humu, jambo fulani kupata,
Ndugu yenu bado nipo, msidhani sipo tena.

Yasinta kapiga simu, kutwa akinitafuta,
Yake ni mang'amung'amu, aliposhindwa nipata,
Akaagiza salamu, yule atayenikuta,
Ndugu yenu bado nipo, msidhani sipo tena.

Kabla kuwa wazimu, Simon kanipata,
Naye ilimlazimu, kunihoji akitweta,
Mtakatifu katimu, hatimaye kunikuta,
Ndugu yenu bado nipo, msidhani sipo tena.

Mzee wa Baragumu, watu wote kawaita,
Changamoto zimo humu, Wavuti zikitokota,
Wengine wote muhimu, njia zote wamepita,
Ndugu yenu bado nipo, msidhani sipo tena.

Leo imenilazimu, kuruka haya matuta,
Kuwaletea salamu, moyoni sijawafuta,
Ninyi kwangu ni muhimu, kwenu furaha napata,
Ndugu yenu bado nipo, msidhani sipo tena.

5 comments:

 1. Twashukuru umerudi nasi furaha tele kwani binafsi nilikumiss, pia niliyamiss mashairi kwani katika mashairi nina udhaifu sana- Ahsante mtani. Na tena hongera

  ReplyDelete
 2. Nasi tupo Mkuu Kijiweni kwako hatukosi!

  ReplyDelete
 3. da Yasinta....kaka Chib na Mtakatifu Simon....ahsanteni sana kwa kutonichoka.

  ReplyDelete
 4. Mtani hakuna mpango wa kuchokana hapa.... na haya mashairi yalivyo matamu we acha tu:-)

  ReplyDelete