Saturday, November 27, 2010

Tanesco mnakera

Tanesco mnakera, ukweli leo nasema,
Mnatutia hasira, kwani hamna huruma,
Mnatutia hasara, ni mbovu yenu huduma,
Kata kata ya umeme, Tanesco mnakera.

Hata huruma hakuna, mwaonesha hamjali,
Umeme mwakata sana, hakuna hata kauli,
Nyie hamna maana, daima siyo wakweli,
Kata kata ya umeme, Tanesco mnakera.

Hakuna maisha bora, Tanesco mwazingua,
Biashara zadorora, vitu vyetu vyaungua,
Nasema kweli mwakera, umeme navyosumbua,
Kata kata ya umeme, Tanesco mnakera.

Sisi wenye masaluni, mwataka tukale wapi?
Tanesco mna nini, kwani bili hatulipi?
Mwatupa umasikini, ama wote twuze pipi?
Kata kata ya umeme, Tanesco mnakera.

Sisi tuuzao maji, Tanesco mwatukera,
Umeme ndiyo mtaji, kwenye yetu biashara,
Lakini hamuhitaji, tupate maisha bora,
Kata kata ya umeme, Tanesco mnakera.

Wale wauza barafu, ama wenye mahoteli,
Wapata uharibifu, nyie wala hamjali,
Huo wenu unyamafu, bora mkafie mbali,
Kaka kata ya umeme, Tanesco mnakera.

Kiujumla mwakera, tena mnatuchefua,
Mwaongeza ufukara, hakya kweli mwatibua,
Hiyo yenu mishahara, ni bora ingepungua,
Kata kata ya umeme, Tanesco mnakera.

Tena mwafanya kusudi, taifa mwalikomoa,
Huo wenu ufisadi, siku moja yawajia,
Hakika itatubidi, vitini kuwaondoa,
Kata kata ya umeme, Tanesco mnakera.

Bora itungwe sheria, wengine waruhusiwe,
Umeme kutuletea, Tanesco mkimbiwe,
Wabunge nyote sikia, twaomba tusaidiwe,
Kata kata ya umeme, Tanesco mnakera.

Rais fanya hatua, ulisafishe shirika,
Wananchi twaumia, limeoza linanuka,
Vitu watuunguzia, utu ulishawatoka,
Kata kata ya umeme, Tanesco mnakera.

Ya kusema nimesema, ujumbe umeshafika,
Tanesco siyo wema, hali ishaharibika,
Siku moja mtakoma, kwani tushakasirika.
Kata kata ya umeme, Tanesco mnakera.

Monday, November 15, 2010

Bado nipo

Sikuishika kalamu, siku nyingi zimepita,
Sikuwapeni salamu, hadi moyo wanipwita,
Sasa napata wazimu, kuhisi mshanifuta,
Ndugu yenu bado nipo, msidhani sipo tena.

Sijui ni majukumu, haya yamenikamata,
Uvivu kwangu ni sumu, wala usingenipata,
Nikatingwa mumu humu, jambo fulani kupata,
Ndugu yenu bado nipo, msidhani sipo tena.

Yasinta kapiga simu, kutwa akinitafuta,
Yake ni mang'amung'amu, aliposhindwa nipata,
Akaagiza salamu, yule atayenikuta,
Ndugu yenu bado nipo, msidhani sipo tena.

Kabla kuwa wazimu, Simon kanipata,
Naye ilimlazimu, kunihoji akitweta,
Mtakatifu katimu, hatimaye kunikuta,
Ndugu yenu bado nipo, msidhani sipo tena.

Mzee wa Baragumu, watu wote kawaita,
Changamoto zimo humu, Wavuti zikitokota,
Wengine wote muhimu, njia zote wamepita,
Ndugu yenu bado nipo, msidhani sipo tena.

Leo imenilazimu, kuruka haya matuta,
Kuwaletea salamu, moyoni sijawafuta,
Ninyi kwangu ni muhimu, kwenu furaha napata,
Ndugu yenu bado nipo, msidhani sipo tena.