Thursday, September 30, 2010

Sijiwezi juu yako

Mwenzako sinayo hali, hali yangu taabani,
Kwako sinayo kauli, ila hisia moyoni,
Hata ninywe dawa kali, hazinifai mwilini,
Sijiwezi juu yako, nipo hoi taabani.

Lolote sijitambui, nakuwaza akilini,
Ninaoza sijijui, we tabibu wa thamani,
Homa hainipungui, kuwa nawe natamani,
Sijiwezi juu yako, nipo hoi taabani.

Pendo langu kwako wewe, latoka mwangu moyoni,
Naomba unielewe, niondoe majonzini,
Yanifanya nichachawe, kukukosa sitamani,
Sijiwezi juu yako, nipo hoi taabani.

Yachanuapo maua, chanua mwangu moyoni,
Furaha inapokua, kuwa nami furahani,
Maana ninaugua, nimeshazama dimbwini,
Sijiwezi juu yako, nipo hoi taabani.

Sitamani kukukosa, nitapatwa na huzuni,
Hakika utanitesa, kama samaki vumbini,
Hisia zinanigusa, nipende basi jamani,
Sijiwezi juu yako, nipo hoi taabani.

Ninayo mang'amung'amu, u dawa usingizini,
Kuwa nawe nina hamu, uniondoe ndotoni,
Ninapatwa na wazimu, chakula sikitamani,
Sijiwezi juu yako, nipo hoi taabani.

Peke yangu sijiwezi, ila uwepo pembeni,
Maisha yana majonzi, wewe langu tumaini,
Mapenzi nitayaenzi, furahani na shidani,
Sijiwezi juu yako, nipo hoi taabani.

Jibu nalisubiria, usinitupe kapuni,
Daima nakuwazia, kila saa duniani,
Pendo ninakupatia, silitupe jalalani,Sijiwezi juu yako, nipo hoi taabani.

4 comments:

 1. Mtani wangu! Nina imani kilio chako kinasikika na ipo siku mtakuwa ubavu kwa ubavu. Na nina imani salam hizi wifi anazipata. Kama mwanamke nina imani leo akisoma hapa hatalala.
  kwani shairi limenigusa kinamna. Mweh! watu wamezaliwa na vipaji, Wifi yangu mtarajiwa ana raha kweli kuyasikia mashairi kama haya kila siku raha sana. Siku yako ipo njiani mpendwa utafurahi, utaweza juu yake na hutakuwa taabani tena.

  ReplyDelete
 2. Wewe ndio moyo wangu, itika basi mpenzi,
  dira ya maisha yangu, bila wewe sijiwezi,
  sogea karibu yangu, unifute langu chozi,
  Njoo tuifunge pingu,niwe wako mjakazi.

  ReplyDelete
 3. if you dont care about yourself sometimes your dont die,but if you care alot about yourself,your kids,wife,husband they will die soon. Mimi siamini katika msemo wa mtu kafa kwa ukwimi au nikitumia kondom sitokufa,mtu anavaa kondom sio kuogo...pa ukimwi bali kifo....if you think sana about yourself you will die....kipindupindu....umewahi kunywa (kwa wale wa nyumbani tu) maji ambayo bata katoka kuyachezea?.........umewahi kupika mchele ambao umechanganywa na vipande vya chupa za soda? umewahi kukaa siku 5 choo hukijui?

  ReplyDelete