Tuesday, September 7, 2010

Utenzi wa asubuhi

Nauandika niamkapo,
Nikutumie huko ulipo,
Daima nikufikiriapo,
Nautamani wako uwepo,
Nijuvye sasa u khali gani?

Asubuhi hii niwazapo,
Wahka moyoni ujaapo,
Natamani karibu uwepo,
Kwani pendo kwako lingalipo,
Wewe furaha yangu moyoni.

Maneno yangu niyasemapo,
Yakufikie kama upepo,
Wakati sauti ivumapo,
Moyo wako ustarehepo,
Nami ninayo raha moyoni.

Tenzi hii nikutumiapo,
Ujuwe kichwani mwangu upo,
Fikra juu yako zijapo,
Ninapenda zizidi kuwepo,
Wewe kwangu unayo thamani.

Mpenzi, nawe ulisomapo,
Uutamani wangu uwepo,
Ndivyo penzi letu likuapo,
Hadi siku pumzi isiwepo,
Nitakupenda toka moyoni.

Hapa mwishoni nikuagapo,
Busu langu likufik'e hapo,
Kwa huba ya pendo lililopo,
Linijazalo raha ya pepo,
U mpenzi wangu wa moyoni.

6 comments:

 1. Naona huu ujumbe umelengwa kwa mtu fulani... lol

  ReplyDelete
 2. Duh! Mtani hapa leo pananoga,
  nahisi kama kaka chib ujumbe huu umemlenga mtu maalum sana (WIFI) halafu umetulia. nimeukuta huu usemi sehemu nikaupenda nawe nakuambia "ukangalage ulimage..."

  ReplyDelete
 3. Ha ha ha haaaa kaka Chib ni kweli kabisa huu ujumbe umelengwa kwake mhusika.

  Da Yasinta ha haaa wifi yako lazima aandikiwe ili ajue namaanisha..
  Ndikangalage nilimage ndilalya humwaya...nikazane nilime nitakula mwakani...

  Ahsanteni sana kwa kutonichoka.

  ReplyDelete
 4. Ni furaha kusikia kuwa ni lazima umwandikie wifi ili ajue unamaanisha. Na mtani, watani huwa hawachokani.

  ReplyDelete
 5. Mkuu kwa kauli nakuamini! Wote tungekuwa na utaalamu wa kauli kama wewe naamini duniani asingebakwa mtu. Ingekuwa kauli tu mpaka kieleweke.:-)

  ReplyDelete
 6. Ha ha ha ha haaaa mtakatifu Simon..nashukuru sana mkuu kwa compliments zako..

  ReplyDelete