Monday, September 13, 2010

Sehemu yangu

Ingali pamoja nawe, sitoacha kukuwaza,
Kuwaza kuhusu wewe, ndicho ninachokiweza,
Siniache nichachawe, mapenzi kuniumiza,
Sehemu yangu i kwako, njoo nitulize moyo.

Mie nakufikiria, hadi ninapitiliza,
Mawazo yanizidia, wewe ndo wa kupunguza,
Sinifanye kuumia, mwenzio utaniliza,
Sehemu yangu i kwako, njoo nitulize moyo.

Moyo wangu nimekupa, usije utelekeza,
Mwenzako ukanitupa, nitakufa nitaoza,
Penzi lako lipo hapa, kwingine watakwumiza,
Sehemu yangu i kwako, njoo nitulize moyo.

Usijali wenye chuki, kamwe hawatotuweza,
Moyo wangu wamiliki, usiache kuutunza,
Kukukosa kwangu dhiki, hakika utaniliza,
Sehemu yangu i kwako, njoo nitulize moyo.

Unayo yangu sehemu, moyo wako kuujaza,
Kwangu una umuhimu, wanifanya kukuwaza,
Kukukosa ninywe sumu, dunia kuishangaza,
Sehemu yangu i kwako, njoo nitulize moyo.

Moyoni nina wahka, uje hima kutuliza,
Yaniondoke mashaka, furaha ukanijaza,
Nahitaji burudika, wewe ndo wa kukoleza,
Sehemu yangu i kwako, njoo nitulize moyo.

3 comments:

 1. Hii ahadi ya wote, tuweke nia moyoni.
  Juma ali na Obote, Asha naye sikudhani
  Nia ikiwa ni sote, adui yu mashakani.
  Tutafikia popote, umoja tukidumisha.

  ReplyDelete
 2. Mtani wala usiwe na shaka siku moja mwenza wako atakuja na mtakuwa pamoja na mtapata watoto ambao wataizunguka meza na mtaishi maisha mema kabisa. Haraka haraka haina baraka...

  ReplyDelete
 3. Mtani jamani
  hakika sisemi
  shairi limeona
  kushiba dona

  ReplyDelete