Thursday, September 30, 2010

Sijiwezi juu yako

Mwenzako sinayo hali, hali yangu taabani,
Kwako sinayo kauli, ila hisia moyoni,
Hata ninywe dawa kali, hazinifai mwilini,
Sijiwezi juu yako, nipo hoi taabani.

Lolote sijitambui, nakuwaza akilini,
Ninaoza sijijui, we tabibu wa thamani,
Homa hainipungui, kuwa nawe natamani,
Sijiwezi juu yako, nipo hoi taabani.

Pendo langu kwako wewe, latoka mwangu moyoni,
Naomba unielewe, niondoe majonzini,
Yanifanya nichachawe, kukukosa sitamani,
Sijiwezi juu yako, nipo hoi taabani.

Yachanuapo maua, chanua mwangu moyoni,
Furaha inapokua, kuwa nami furahani,
Maana ninaugua, nimeshazama dimbwini,
Sijiwezi juu yako, nipo hoi taabani.

Sitamani kukukosa, nitapatwa na huzuni,
Hakika utanitesa, kama samaki vumbini,
Hisia zinanigusa, nipende basi jamani,
Sijiwezi juu yako, nipo hoi taabani.

Ninayo mang'amung'amu, u dawa usingizini,
Kuwa nawe nina hamu, uniondoe ndotoni,
Ninapatwa na wazimu, chakula sikitamani,
Sijiwezi juu yako, nipo hoi taabani.

Peke yangu sijiwezi, ila uwepo pembeni,
Maisha yana majonzi, wewe langu tumaini,
Mapenzi nitayaenzi, furahani na shidani,
Sijiwezi juu yako, nipo hoi taabani.

Jibu nalisubiria, usinitupe kapuni,
Daima nakuwazia, kila saa duniani,
Pendo ninakupatia, silitupe jalalani,Sijiwezi juu yako, nipo hoi taabani.

Thursday, September 23, 2010

Nafikiri

Akili si huru tena,
I mzigoni ikitafakari,
Ya leo ama ya kesho,
Ya mustakabali.
Mbiu ishapigwa,
Kitambo sasa.
Si ya mavuvuzela,
Bali ya awamu na dawamu.

Mwalimu darasani,
Alishasema,
Kupanga ni kuchagua.

Mahotma akatuambia,
Tuwe yale,
Mabadiliko,
Ambayo tungependa,
Kuyaona,
Duniani.

Sheikh Ebrahim Hussein,
Akainunua saa yake,
Alipoitazama vema,
Hakusita kusema,
Wakati ni Ukuta.

Namfikiria tena,
Mwanamapinduzi yule,
Bob Marley,
Kwa nini alisema,
Wakati Utaongea.
Kwa nini lakini,
Kazi ipo!

Msakatonge,
Mohamed Seif Khatib,
Akasema,
Hatukubali.
Kuja tena ili kuonewa,
Ndani ya nchi yetu,
Iliyo huru.

Akaja naye Ustaadh,
Khamis Amani,
Nyamaume,
Yeye akasema,
Mjinga mpe kilemba,
Mbele akutangulie.

Jinamizi bado laja,
La Ali Salim Zakwany,
Manenoye kugongana,
Bue silione bue,
La taji na buibui.

Nafikiri!

Monday, September 13, 2010

Sehemu yangu

Ingali pamoja nawe, sitoacha kukuwaza,
Kuwaza kuhusu wewe, ndicho ninachokiweza,
Siniache nichachawe, mapenzi kuniumiza,
Sehemu yangu i kwako, njoo nitulize moyo.

Mie nakufikiria, hadi ninapitiliza,
Mawazo yanizidia, wewe ndo wa kupunguza,
Sinifanye kuumia, mwenzio utaniliza,
Sehemu yangu i kwako, njoo nitulize moyo.

Moyo wangu nimekupa, usije utelekeza,
Mwenzako ukanitupa, nitakufa nitaoza,
Penzi lako lipo hapa, kwingine watakwumiza,
Sehemu yangu i kwako, njoo nitulize moyo.

Usijali wenye chuki, kamwe hawatotuweza,
Moyo wangu wamiliki, usiache kuutunza,
Kukukosa kwangu dhiki, hakika utaniliza,
Sehemu yangu i kwako, njoo nitulize moyo.

Unayo yangu sehemu, moyo wako kuujaza,
Kwangu una umuhimu, wanifanya kukuwaza,
Kukukosa ninywe sumu, dunia kuishangaza,
Sehemu yangu i kwako, njoo nitulize moyo.

Moyoni nina wahka, uje hima kutuliza,
Yaniondoke mashaka, furaha ukanijaza,
Nahitaji burudika, wewe ndo wa kukoleza,
Sehemu yangu i kwako, njoo nitulize moyo.

Tuesday, September 7, 2010

Utenzi wa asubuhi

Nauandika niamkapo,
Nikutumie huko ulipo,
Daima nikufikiriapo,
Nautamani wako uwepo,
Nijuvye sasa u khali gani?

Asubuhi hii niwazapo,
Wahka moyoni ujaapo,
Natamani karibu uwepo,
Kwani pendo kwako lingalipo,
Wewe furaha yangu moyoni.

Maneno yangu niyasemapo,
Yakufikie kama upepo,
Wakati sauti ivumapo,
Moyo wako ustarehepo,
Nami ninayo raha moyoni.

Tenzi hii nikutumiapo,
Ujuwe kichwani mwangu upo,
Fikra juu yako zijapo,
Ninapenda zizidi kuwepo,
Wewe kwangu unayo thamani.

Mpenzi, nawe ulisomapo,
Uutamani wangu uwepo,
Ndivyo penzi letu likuapo,
Hadi siku pumzi isiwepo,
Nitakupenda toka moyoni.

Hapa mwishoni nikuagapo,
Busu langu likufik'e hapo,
Kwa huba ya pendo lililopo,
Linijazalo raha ya pepo,
U mpenzi wangu wa moyoni.