Sunday, August 8, 2010

Kwa nini?

Ninatazama pembeni, mwingine hata simwoni,
Nauliza kulikoni, swali labaki moyoni,
Atayenijibu nani, jibu ninalitamani,
Kwa nini nina upweke?

Natazama kitandani, kwanza juu kisha chini,
Natazama mlangoni, kisha kule ukutani,
Labda yupo darini, lakini afwate nini,
Kwa nini nina upweke?

Ninakwenda koridoni, lakini bado simwoni,
Haya yataisha lini, upweke siutamani,
Aje, aje, aje nani, anitoe simanzini,
Kwa nini nina upweke?

Natazama sebuleni, yeyote haonekani,
Nafika hata jikoni, sioni kitu jamani,
Machozi sasa machoni, atayeyafuta nani,
Kwa nini nina upweke?

Nakwenda barabarani, nafika hadi mjini,
Ninaranda mitaani, nijifariji moyoni,
Mawazo tele kichwani, upweke tatoka lini,
Kwa nini nina upweke?

Nilipo ni ugenini, upweke mwangu moyoni,
Raha ninayotamani, wewe uwepo pembeni,
Sitaki hii huzuni, ilonitupa dimbwini,
Sitaki tena upweke.

4 comments:

 1. Kilio chako bayana, chahitaji mwanandani
  Umtafute kila kona, ipo siku utawini
  Na hii katupa rabana, wewe huwezi kuhini.
  kuishi mke na mume, upweke hutouona.

  ReplyDelete
 2. Usikate tamaa, utampata tu tena atakuwa mke mwema kwako. Na mtaishi maisha ya raha na huo upweke utaisha. Maisha ni polepole haraka haraka haina baraka.

  ReplyDelete
 3. Upweke kweli kuishi bila ushairi
  Nimekaa sana bila kuweka maneno matamu akilini
  Nimeyapata hapa kwa diwani ya fadhili
  Sasa nitembelee Yasinta..nione mapya ni nini

  ReplyDelete