Monday, August 30, 2010

Furaha yangu

Furaha yangu moyoni,
Ni pendo'lo la thamani,
Sitochagua huzuni.

Raha yangu maishani,
Wewe uwepo pembeni,
Chakula changu rohoni.

Moyoni nakutamani,
Mwongozo wangu njiani,
Nahodha mwema chomboni.

Wewe ndiwe duniani,
Mwenye kuvaa nishani,
Tuwashinde wafitini.

Maneno yako laini,
Kinanda masikioni,
Na utamu mdomoni.

Pekee ulimwenguni,
Uiletaye amani,
Kun'suza mtimani.

U ndoto usingizini,
Fikra zangu kichwani,
Furaha yangu moyoni.

1 comment:

 1. nanukuu " U ndoto usingizini,
  Fikra zangu kichwani,
  Furaha yangu moyoni." mwisho wa kunukuu

  Furaha ni muhimu katika maisha,
  Upendo pia thamani
  Kuwa na wako pembeni.
  Hakuna asiyependa.
  Furaha, upendo,raha na amani.

  ReplyDelete