Monday, August 30, 2010

Furaha yangu

Furaha yangu moyoni,
Ni pendo'lo la thamani,
Sitochagua huzuni.

Raha yangu maishani,
Wewe uwepo pembeni,
Chakula changu rohoni.

Moyoni nakutamani,
Mwongozo wangu njiani,
Nahodha mwema chomboni.

Wewe ndiwe duniani,
Mwenye kuvaa nishani,
Tuwashinde wafitini.

Maneno yako laini,
Kinanda masikioni,
Na utamu mdomoni.

Pekee ulimwenguni,
Uiletaye amani,
Kun'suza mtimani.

U ndoto usingizini,
Fikra zangu kichwani,
Furaha yangu moyoni.

Sunday, August 15, 2010

Nishike mkono

Upweke unaponiandama,
Nami kukosa pa kuegama,
Bado nahitaji usalama,
Hata tufani linapovuma,
Ninaponywa nalo neno jema,
Maana sitochoka mapema,
Ni sauti yenye kuchombeza,
Niipendayo kuisikiliza,
Dunia inaponiumiza,
Peke yangu mimi sitoweza,
Nishike mkono.

Sunday, August 8, 2010

Kwa nini?

Ninatazama pembeni, mwingine hata simwoni,
Nauliza kulikoni, swali labaki moyoni,
Atayenijibu nani, jibu ninalitamani,
Kwa nini nina upweke?

Natazama kitandani, kwanza juu kisha chini,
Natazama mlangoni, kisha kule ukutani,
Labda yupo darini, lakini afwate nini,
Kwa nini nina upweke?

Ninakwenda koridoni, lakini bado simwoni,
Haya yataisha lini, upweke siutamani,
Aje, aje, aje nani, anitoe simanzini,
Kwa nini nina upweke?

Natazama sebuleni, yeyote haonekani,
Nafika hata jikoni, sioni kitu jamani,
Machozi sasa machoni, atayeyafuta nani,
Kwa nini nina upweke?

Nakwenda barabarani, nafika hadi mjini,
Ninaranda mitaani, nijifariji moyoni,
Mawazo tele kichwani, upweke tatoka lini,
Kwa nini nina upweke?

Nilipo ni ugenini, upweke mwangu moyoni,
Raha ninayotamani, wewe uwepo pembeni,
Sitaki hii huzuni, ilonitupa dimbwini,
Sitaki tena upweke.