Saturday, July 10, 2010

Wataka tena nafasi

Maneno nimesikia, ninayo mwangu moyoni,
Yote unayonambia, natafakari kichwani,
Endelea subiria, jawabu lipo mbioni,
Wataka kwangu nafasi, ya mwanzo ulichezea.

Wataka nifikirie, ili nikupe nafasi,
Jawabu nikupatie, ukuishe wasiwasi,
Yafanya unililie, nitoe jibu upesi,
Wataka kwangu nafasi, ya mwanzo ulichezea.

Ya kwanza ulichezea, nafasi niliyokupa,
Nyodo ukailetea, mwishowe ukaitupa,
Sasa unaitetea, hutaki kutoka kapa,
Wataka kwangu nafasi, ya mwanzo ulichezea.

Lakini nilikwambia, tena kwa wangu mdomo,
Hamna hamna pia, basi ndimo mliwamo,
Wewe hukufikiria, maana yake msemo,
Wataka kwangu nafasi, ya mwanzo ulichezea.

Ukishataka kuruka, basi agana na nyonga,
Siyo unakurupuka, kisha mwamba unagonga,
Halafu walalamika, wasema ninakutenga,
Wataka kwangu nafasi, ya mwanzo ulichezea.

Ganda la muwa la jana, chungu kaona kivuno,
Taamali kwayo kina, kichwani lipime neno,
Moyo si wa kuuchana, vipande viwili hino,
Wataka kwangu nafasi, ya mwanzo ulichezea.

Eti miaka mingine, hii haijakutosha,
Nitalie chako kine, si maneno kujikosha,
Wepishwe walo wengine, chombo kicho kukiosha,
Wataka kwangu nafasi, ya mwanzo ulichezea.

4 comments:

 1. Wapi ulipokuwepo, nini kimekurudisha,
  Umekuja ka upepo,wangu moyo watingisha,
  Nipe muda ninawaza, jibu nitakupatia.


  Kipi kilichokusibu, mpaka ukaondoka,
  Nijuze tatu sababu, kwa nini kunikumbuka,
  Leo waja kwa adabu, waonyesha kutukuka.
  Nipe muda nawaza, jibu nitakupatia.


  Wataka kunirudia, kulikoni utokako,
  Yupo ulo mkimbia,tabia hii ni yako,
  Nipe muda nawaza, jibu nitakupatia.

  ReplyDelete
 2. Nadhani huyo mtu inabidi asema SAMAHANI!

  ReplyDelete
 3. Kissima ulilosema, ni jambo limetulia,
  Nimeona ni mapema, haya nikamwandikia,
  Ili aweze kupima, ukweli kujionea.

  Yasinta wanisikia, ulisome somo vema,
  Kisha 'tanisaidia, ninataka kukutuma,
  Haya nenda kumwambia, kwa staha na hekima.

  ReplyDelete
 4. Kaka unajitaidi,kupa mkono yabudi
  nashanga hao fisadi,wao kuponda kusudi

  ReplyDelete