Sunday, July 4, 2010

Mimi huyu

Muda sasa umepita, bila ya kunisikia,
Lipi lililo nipata, maswali yanawajia,
Ni vipi imenikuta, hata nikawapotea.

Ama kombe la dunia, muda wangu lamaliza,
Mbona sikuwaambia, tuseme nimeteleza,
Tungo kutowaletea, hakika ninawakwaza.

Mwenyewe nimefikiri, kwa marefu na mapana,
Nikaona si vizuri, hewani kukosekana,
Kutoandika shairi, hewani kuonekana.

Leo nimedhamiria, haya niwaambieni,
Mpate kunisikia, kwa radhi kuwatakeni,
Hakika sitorudia, bure mnisameheni.

Ushairi Kiswahili, ni kitu nikipendacho,
Titi la mama kamili, chakula kishibishacho,
Nanyi mnastahili, chema kasoro sicho.

1 comment:

  1. Ni furaha ilioje kuweza kusoma tena mashairi yako mtani kweli ulipotea na nilikuwa najiuliza kulikon. Ahsante sana shairi limetulia yaani bombi kweli, karibu tena:-)

    ReplyDelete