Thursday, July 15, 2010

Lazima tusonge mbele

Magumu hututokea, tena yakatuumiza,
Mizigo kutwelemea, kiasi cha kutuliza,
Tamaa twajikatia, kuhisi twajipoteza,
Lazima tusonge mbele.

Mabaya yanatupata, tena yenye kuzidia,
Nasi tunajikunyata, na pengine tunalia,
Simanzi napojikita, kushindwa kuvumilia,
Lazima tusonge mbele.

Mambo yanapotokea, waweza tamani sumu,
Hujui pa kushikia, wala wa kumlaumu,
Mambo kuharibikia, hata kuleta wazimu,
Lazima tusonge mbele.

Unakosa pa kushika, na nani umlilie,
Unabaki kuteseka, marafiki wakimbie,
Moyo wako wapondeka, nani akusaidie,
Lazima tusonge mbele.

Dunia siyo ya kwetu, wala si mteremko,
Dunia inao watu, wengine wenye vituko,
Wapo na roho za kutu, kuumiza moyo wako,
Lazima tusonge mbele.

Dunia ni majaribu, dunia ni mitihani,
Dunia inaharibu, mawazo ya akilini,
Vema kujua wajibu, Mola kumtumaini,
Lazima tusonge mbele.

Lazima tukaze moyo, maisha yaendelee,
Ili yale tupatayo, hasi yasituletee,
Imani yaivunjayo, papa hapa yakomee,
Lazima tusonge mbele.

Lazima tujifariji, tuna mengi ya kufanya,
Ni kweli tu wahitaji, na shida hutuchanganya,
Na Mola ndiye mpaji, kwingine twajidanganya,
Lazima tusonge mbele.

Lazima tukapambane, mkono kwao mkono,
Ushindi upatikane, tena ulio mnono,
Simanzi tuondokane, maumivu ya sindano,
Lazima tusonge mbele.

Tuwashinde wafitini, kwa moyo nayo dhamira,
Lakini tuwe makini, tutangulize busara,
Ili tusirudi chini, tuwe juu ya mnara,
Lazima tusonge mbele.

Tukawe wavumilivu, tukipatwa na mikasa,
Tuyashinde maumivu, furaha tunapokosa,
Mikono kuwa mikavu, na kushindwa kupapasa,
Lazima tusonge mbele.

Zinatosha beti hizi, zishafikia dazeni,
Bila ya Mola siwezi, kuyavuka salimini,
Maana ndiye mwokozi, dereva wangu chomboni,
Lazima nisonge mbele.Wakati wote hupenda kuandika mashairi juu ya watu wengine. Kueleza furaha, upendo, urafiki, imani na huzuni. Lakini mambo hugeuka. Leo nimeandika shairi maalumu kwa ajili ya Fadhy Mtanga, baada ya kupambana na kipindi kigumu sana kwa takribani mwezi mzima. Alipokumbuka anapaswa kuacha kujishika kichwa, leo nikamwandikia shairi kumkumbusha LAZIMA ASONGE MBELE...kaniahidi anasonga....kwa kuwa Mungu ni Mwema.

2 comments:

 1. nanukuu "Mambo yanapotokea, waweza tamani sumu,
  Hujui pa kushikia, wala wa kumlaumu,
  Mambo kuharibikia, hata kuleta wazimu,
  Lazima tusonge mbele." mwisho wa kunikuu
  Nimesoma shairi hili na limenisisimua kwa kuona kumbe unaweza kujiandikia shairi mwenyewe na pia linasikitisha je mtani nini kinakusibu?

  ReplyDelete