Thursday, July 15, 2010

Lazima tusonge mbele

Magumu hututokea, tena yakatuumiza,
Mizigo kutwelemea, kiasi cha kutuliza,
Tamaa twajikatia, kuhisi twajipoteza,
Lazima tusonge mbele.

Mabaya yanatupata, tena yenye kuzidia,
Nasi tunajikunyata, na pengine tunalia,
Simanzi napojikita, kushindwa kuvumilia,
Lazima tusonge mbele.

Mambo yanapotokea, waweza tamani sumu,
Hujui pa kushikia, wala wa kumlaumu,
Mambo kuharibikia, hata kuleta wazimu,
Lazima tusonge mbele.

Unakosa pa kushika, na nani umlilie,
Unabaki kuteseka, marafiki wakimbie,
Moyo wako wapondeka, nani akusaidie,
Lazima tusonge mbele.

Dunia siyo ya kwetu, wala si mteremko,
Dunia inao watu, wengine wenye vituko,
Wapo na roho za kutu, kuumiza moyo wako,
Lazima tusonge mbele.

Dunia ni majaribu, dunia ni mitihani,
Dunia inaharibu, mawazo ya akilini,
Vema kujua wajibu, Mola kumtumaini,
Lazima tusonge mbele.

Lazima tukaze moyo, maisha yaendelee,
Ili yale tupatayo, hasi yasituletee,
Imani yaivunjayo, papa hapa yakomee,
Lazima tusonge mbele.

Lazima tujifariji, tuna mengi ya kufanya,
Ni kweli tu wahitaji, na shida hutuchanganya,
Na Mola ndiye mpaji, kwingine twajidanganya,
Lazima tusonge mbele.

Lazima tukapambane, mkono kwao mkono,
Ushindi upatikane, tena ulio mnono,
Simanzi tuondokane, maumivu ya sindano,
Lazima tusonge mbele.

Tuwashinde wafitini, kwa moyo nayo dhamira,
Lakini tuwe makini, tutangulize busara,
Ili tusirudi chini, tuwe juu ya mnara,
Lazima tusonge mbele.

Tukawe wavumilivu, tukipatwa na mikasa,
Tuyashinde maumivu, furaha tunapokosa,
Mikono kuwa mikavu, na kushindwa kupapasa,
Lazima tusonge mbele.

Zinatosha beti hizi, zishafikia dazeni,
Bila ya Mola siwezi, kuyavuka salimini,
Maana ndiye mwokozi, dereva wangu chomboni,
Lazima nisonge mbele.Wakati wote hupenda kuandika mashairi juu ya watu wengine. Kueleza furaha, upendo, urafiki, imani na huzuni. Lakini mambo hugeuka. Leo nimeandika shairi maalumu kwa ajili ya Fadhy Mtanga, baada ya kupambana na kipindi kigumu sana kwa takribani mwezi mzima. Alipokumbuka anapaswa kuacha kujishika kichwa, leo nikamwandikia shairi kumkumbusha LAZIMA ASONGE MBELE...kaniahidi anasonga....kwa kuwa Mungu ni Mwema.

Saturday, July 10, 2010

Wataka tena nafasi

Maneno nimesikia, ninayo mwangu moyoni,
Yote unayonambia, natafakari kichwani,
Endelea subiria, jawabu lipo mbioni,
Wataka kwangu nafasi, ya mwanzo ulichezea.

Wataka nifikirie, ili nikupe nafasi,
Jawabu nikupatie, ukuishe wasiwasi,
Yafanya unililie, nitoe jibu upesi,
Wataka kwangu nafasi, ya mwanzo ulichezea.

Ya kwanza ulichezea, nafasi niliyokupa,
Nyodo ukailetea, mwishowe ukaitupa,
Sasa unaitetea, hutaki kutoka kapa,
Wataka kwangu nafasi, ya mwanzo ulichezea.

Lakini nilikwambia, tena kwa wangu mdomo,
Hamna hamna pia, basi ndimo mliwamo,
Wewe hukufikiria, maana yake msemo,
Wataka kwangu nafasi, ya mwanzo ulichezea.

Ukishataka kuruka, basi agana na nyonga,
Siyo unakurupuka, kisha mwamba unagonga,
Halafu walalamika, wasema ninakutenga,
Wataka kwangu nafasi, ya mwanzo ulichezea.

Ganda la muwa la jana, chungu kaona kivuno,
Taamali kwayo kina, kichwani lipime neno,
Moyo si wa kuuchana, vipande viwili hino,
Wataka kwangu nafasi, ya mwanzo ulichezea.

Eti miaka mingine, hii haijakutosha,
Nitalie chako kine, si maneno kujikosha,
Wepishwe walo wengine, chombo kicho kukiosha,
Wataka kwangu nafasi, ya mwanzo ulichezea.

Sunday, July 4, 2010

Mimi huyu

Muda sasa umepita, bila ya kunisikia,
Lipi lililo nipata, maswali yanawajia,
Ni vipi imenikuta, hata nikawapotea.

Ama kombe la dunia, muda wangu lamaliza,
Mbona sikuwaambia, tuseme nimeteleza,
Tungo kutowaletea, hakika ninawakwaza.

Mwenyewe nimefikiri, kwa marefu na mapana,
Nikaona si vizuri, hewani kukosekana,
Kutoandika shairi, hewani kuonekana.

Leo nimedhamiria, haya niwaambieni,
Mpate kunisikia, kwa radhi kuwatakeni,
Hakika sitorudia, bure mnisameheni.

Ushairi Kiswahili, ni kitu nikipendacho,
Titi la mama kamili, chakula kishibishacho,
Nanyi mnastahili, chema kasoro sicho.