Tuesday, June 8, 2010

Ukimya wangu

Siku zazidi kimbia, nawe hujanisikia,
Najua unaumia, vibaya wajisikia,
Wahisi nakukimbia, upendo umepungua.

Simu ukinipigia, nashindwa kuzipokea,
Mambo yananizidia, nawe huko waumia,
Ninahisi unalia, hujui pa kushikia.

Meseji wanitumia, nashindwa kuzijibia,
Nyingi sana zanijia, siwezi kuhesabia,
Najua wanizimia, nami nakupenda pia.

Kweli wanivumilia, mwingine ‘ngeshakimbia,
Hatiya najisikia, haya nayokufanyia,
Sipendi ukiumia, ni mambo yamezidia.

Si punde nitatulia, nawe utafurahia,
Machozi unayolia, kicheko kitakujia,
Mpenzi wangu tulia, kwako ningali na nia.

Bado nakufikiria, moyoni umenijaa,
Bado ninakuzimia, mwingine hajanifaa,
Unimulikie njia, kwangu uwe ndiye taa.

Upunguze kuumia, sipendi kukuchunia,
Basi uwache kulia, si punde nitatulia,
Mazuri twapigania, ndani ya hii dunia.

3 comments:

  1. Nimesoma Shairi,ama kweli huyo uiyemwandikia kama atasoma hapa atadondosha mchozi zaidi. Maana mimi tu nimedondosha. Pole na kazi mtani.nadhani ujumbe umeshamfikia....

    ReplyDelete
  2. Duh! umelenga kwenyewe.

    mamaa kaza buti rijamaa bado rinakumaindi :-)

    ReplyDelete