Wednesday, June 23, 2010

Tenda wema

Kuna wengi walimwengu, kujaa dunia nzima,
Muumba ni yeye Mungu, kila moja na karama,
Wenye maisha machungu, huhitaji tendwa mema,
Tenda wema nenda zako.

Wale walio shidani, kamwe sije watupa,
Waondoe majonzini, usijaribu wakwepa,
Wafanye was'ende chini, maisha wakaogopa,
Tenda wema nenda zako.

Yale walopungukiwa, ambayo wewe unayo,
Usisite kuyatowa, kadiri uyawezayo,
Upate kuwaokowa, yale yawasumbuayo,
Tenda wema nenda zako.

Wale walio na njaa, usisite kuwalisha,
Waso nguo za kuvaa, ukapate kuwavisha,
Waliokata tamaa, imani kuwahuisha,
Tenda wema nenda zako.

Wale wanaoumia, ukawafute machozi,
Ili waache kulia, wayahimili majonzi,
Hao 'sije wakimbia, peke yao hawawezi'
Tenda wema nenda zako.

Ila utendapo wema, usingoje shukurani,
Tena 'sigeuke nyuma, ungoje kitu fulani,
Tena usije kupima, ujuwe yake thamani,
Tenda wema nenda zako.

Kamwe usihesabu, Mungu ndiye anajuwa,
Kwa hilo ukawe bubu, nawe utabarikiwa,
Timiza wako wajibu, moyo kutopungukiwa,
Tenda wema nenda zako.

4 comments:

 1. Usingoje shukurani, tenda wema wende zako,
  Katu usiangalie nyuma, kutaka kutambuliwa,
  Mola ndiye ajuae, lile jema ulotenda,
  Kutimiza wako wajibu, hiyo ndiyo yako shani,
  Tenda wema nenda zako...........

  ReplyDelete
 2. Maisara we ni mshairi mzuri sana. Hongera sana.

  Da Yasinta ahsante sana kwa kutonichoka

  ReplyDelete