Friday, June 11, 2010

Njoo kwangu

Raha tele ikihitajika,
Mabonde na milima kuvuka,
Kuufanya moyo kukongeka,
Mtima wako kuburudika,
Nafsi nayo ikasuuzika,
Njoo kwangu!

Wataka kusahau huzuni,
Ujawe furaha maishani,
Uifahamu yako thamani,
Utunzwe moyoni na mwilini,
Ili wengine usitamani,
Njoo kwangu!

Wataka sikia neno jema,
La awezaye ishusha homa,
Awezaye ukuna mtima,
Ukapande juu ya mlima,
Kileleni nawe kusimama,
Njoo kwangu!

Yalo matamu utaambiwa,
Yenye mahaba kufurahiwa,
Yalojaa raha kunogewa,
Yaso na kipimo utapewa,
Wala huhitaji simuliwa,
Njoo kwangu!

1 comment:

  1. Ni furaha na raha isiyoweza kuelezeka kuamka asubuhi hii na kuingia hapa kwa Diwani ya Fadhli na kusoma mashairi yake hata kama amemwandikia wake mtarajiwa. Upendo Daima

    ReplyDelete