Wednesday, June 16, 2010

Mtoto wa Afrika

Upo huko mashambani,
Kwenye mazingira duni,
Nani anakuthamini,
Akupeleke shuleni?
Mtoto wa Afrika!

Wahenyeka migodini,
Umezama taabuni,
Hunayo matumaini,
Hujui ‘takula nini,
Mtoto wa Afrika!

Unateseka vitani,
Na bunduki mabegani,
Wanakufundisha nini,
Maisha yako usoni?
Mtoto wa Afrika!

Watendwa mwako mwilini,
Na jitu zima fulani,
La miaka hamsini,
Ukimbilie kwa nani?
Mtoto wa Afrika!

Waondolewa shuleni,
Ukaolewe mjini,
Nani anakuthamini,
Akubakize shuleni?
Mtoto wa Afrika!

Mahali barabarani,
Una kopo mkononi,
U ombaomba jamani,
Sisi wala hatukwoni,
Mtoto wa Afrika!

Wasikia radioni,
Wenzako matamashani,
Na viongozi fulani,
Umebaki mtaani,
Mtoto wa Afrika!

Uliko ni kijijini,
Shuleni waketi chini,
Wenzako huku mjini,
Leo wapo jukwaani,
Mtoto wa Afrika!

Utangoja hadi lini?
Tateseka hadi lini?
Utakombolewa lini?
Utafurahia lini?
Mtoto wa Afrika!

Majibu anayo nani?
Mtoto yupo shidani,
Anakula jalalani,
Twapaswa kumthamini,
Mtoto wa Afrika!

Kwani tunafanya nini?
Na kwa faida ya nani?
Tunajenga kitu gani,
Pasipo kumthamini?
Mtoto wa Afrika!

Tupo usingizini,
Tuamke sasa!

4 comments:

 1. jamani my FM...i never knew una kitu kama hiki yaani nimefurahii kuliko jinsi navyoelezea mungu akubariki sana katika hili nami niko pamoja nawe naona ulichokiandaa ndio kilio halisi cha mtoto wa africa hope tutajifunza mengi kupitia mashairi haya ya mtoto wa Africa...

  thanx sooo much..
  ni mimi mdau wako AH

  ReplyDelete
 2. Nanukuu"Utangoja hadi lini?
  Tateseka hadi lini?
  Utakombolewa lini?
  Utafurahia lini?
  Mtoto wa Afrika"mwisho wa kunukuu:- ni kweli kabisa sasa ni wakati wa kuamka nduguzanguni. Asante kwa shairi hili.

  ReplyDelete
 3. Kaka Chacha bora we ushaamka.

  AH karibu sana na ahsante sana kwa kuzuru kibarazani hapa. tafadhali usichoke kabisa.

  da Yasinta ahsante tena na tena kwa kutonichoka.

  fadhy mtanga

  ReplyDelete