Thursday, June 3, 2010

Hepi bethidei Erik

Mtoto mzuri Erik,
Twamwoma Mungu akubariki,
Akulinde katika mikiki,
Ndani ya hii dunia.

Mungu akupe afya njema,
Akwepushie mbali homa,
Akubariki katika kusoma,
Akili zaidi kukujalia.

Akufanye mtoto mzuri,
Kwa wazazi uwe johari,
Nao wakwonee fahari,
Kama maua ukachanua.

Daima akujalie busara,
Ili usiwe nazo papara,
Wala mtu mwenye hasira,
Bali mwenye kutulia.

Uwe mtu mpatanishi,
Daima pawapo ubishi,
Jiepushe ulalamishi,
Dunia utaifurahia.

Ujaaliwe upendo tele,
Nyumbani nako shule,
Usiwatenge watu wale,
Wala kuwachukia.

Uwe mtu wa sala,
Hata kabla ya kulala,
Na wakati wako wa kula,
Uwaombee wenye njaa.

U kama jemedari,
Kwa wako umahiri,
Simama kwenye mstari,
Mungu atakusimamia.

Heri ya siku ya kuzaliwa,
Maisha marefu utapewa,
Daima unaombewa,
Na mema tunakutakia.

Wasalaam,
Anko Fadhy.

4 comments:

 1. Sijui nilie au nicheke kwa furaha na heshima hii aliyopewa mwanangu. Kuandikiwa shairi na mjomba wake kwa kwa kweli nimeishiwa hata la kusema ila tu nasema ahsante sana. Ni shairi zuri na lenye ujumbe mzuri sana. Ahsante Mtani.

  ReplyDelete
 2. Asante mjomba kwa shairi nzuri!

  ReplyDelete
 3. Watu na vipaji vyao bwana! Hivi hili shairi sijui limekuchukua muda gani kuliandaa. Erik una bahati sana sala uliyoombewa si mchezo. Mimi naomba yote aliyoyaomba Mjomba Fadhy yawe hivyo, AMEN.

  ReplyDelete
 4. Ahsante sana da Yasinta.
  Erik shukrani kwa shukrani zako. Ubarikiwe.
  Da Mija ahsante kwa pongezi zako. Hata mie sijajua exactly nilitumia muda gani kuandika. Ila nilikuwa ndani ya daladala Magomeni hadi Shekilango ikawa kwishney. Tunamshukuru Mungu kwa karama hii.

  ReplyDelete