Wednesday, June 23, 2010

Tenda wema

Kuna wengi walimwengu, kujaa dunia nzima,
Muumba ni yeye Mungu, kila moja na karama,
Wenye maisha machungu, huhitaji tendwa mema,
Tenda wema nenda zako.

Wale walio shidani, kamwe sije watupa,
Waondoe majonzini, usijaribu wakwepa,
Wafanye was'ende chini, maisha wakaogopa,
Tenda wema nenda zako.

Yale walopungukiwa, ambayo wewe unayo,
Usisite kuyatowa, kadiri uyawezayo,
Upate kuwaokowa, yale yawasumbuayo,
Tenda wema nenda zako.

Wale walio na njaa, usisite kuwalisha,
Waso nguo za kuvaa, ukapate kuwavisha,
Waliokata tamaa, imani kuwahuisha,
Tenda wema nenda zako.

Wale wanaoumia, ukawafute machozi,
Ili waache kulia, wayahimili majonzi,
Hao 'sije wakimbia, peke yao hawawezi'
Tenda wema nenda zako.

Ila utendapo wema, usingoje shukurani,
Tena 'sigeuke nyuma, ungoje kitu fulani,
Tena usije kupima, ujuwe yake thamani,
Tenda wema nenda zako.

Kamwe usihesabu, Mungu ndiye anajuwa,
Kwa hilo ukawe bubu, nawe utabarikiwa,
Timiza wako wajibu, moyo kutopungukiwa,
Tenda wema nenda zako.

Wednesday, June 16, 2010

Mtoto wa Afrika

Upo huko mashambani,
Kwenye mazingira duni,
Nani anakuthamini,
Akupeleke shuleni?
Mtoto wa Afrika!

Wahenyeka migodini,
Umezama taabuni,
Hunayo matumaini,
Hujui ‘takula nini,
Mtoto wa Afrika!

Unateseka vitani,
Na bunduki mabegani,
Wanakufundisha nini,
Maisha yako usoni?
Mtoto wa Afrika!

Watendwa mwako mwilini,
Na jitu zima fulani,
La miaka hamsini,
Ukimbilie kwa nani?
Mtoto wa Afrika!

Waondolewa shuleni,
Ukaolewe mjini,
Nani anakuthamini,
Akubakize shuleni?
Mtoto wa Afrika!

Mahali barabarani,
Una kopo mkononi,
U ombaomba jamani,
Sisi wala hatukwoni,
Mtoto wa Afrika!

Wasikia radioni,
Wenzako matamashani,
Na viongozi fulani,
Umebaki mtaani,
Mtoto wa Afrika!

Uliko ni kijijini,
Shuleni waketi chini,
Wenzako huku mjini,
Leo wapo jukwaani,
Mtoto wa Afrika!

Utangoja hadi lini?
Tateseka hadi lini?
Utakombolewa lini?
Utafurahia lini?
Mtoto wa Afrika!

Majibu anayo nani?
Mtoto yupo shidani,
Anakula jalalani,
Twapaswa kumthamini,
Mtoto wa Afrika!

Kwani tunafanya nini?
Na kwa faida ya nani?
Tunajenga kitu gani,
Pasipo kumthamini?
Mtoto wa Afrika!

Tupo usingizini,
Tuamke sasa!

Friday, June 11, 2010

Njoo kwangu

Raha tele ikihitajika,
Mabonde na milima kuvuka,
Kuufanya moyo kukongeka,
Mtima wako kuburudika,
Nafsi nayo ikasuuzika,
Njoo kwangu!

Wataka kusahau huzuni,
Ujawe furaha maishani,
Uifahamu yako thamani,
Utunzwe moyoni na mwilini,
Ili wengine usitamani,
Njoo kwangu!

Wataka sikia neno jema,
La awezaye ishusha homa,
Awezaye ukuna mtima,
Ukapande juu ya mlima,
Kileleni nawe kusimama,
Njoo kwangu!

Yalo matamu utaambiwa,
Yenye mahaba kufurahiwa,
Yalojaa raha kunogewa,
Yaso na kipimo utapewa,
Wala huhitaji simuliwa,
Njoo kwangu!

Tuesday, June 8, 2010

Ukimya wangu

Siku zazidi kimbia, nawe hujanisikia,
Najua unaumia, vibaya wajisikia,
Wahisi nakukimbia, upendo umepungua.

Simu ukinipigia, nashindwa kuzipokea,
Mambo yananizidia, nawe huko waumia,
Ninahisi unalia, hujui pa kushikia.

Meseji wanitumia, nashindwa kuzijibia,
Nyingi sana zanijia, siwezi kuhesabia,
Najua wanizimia, nami nakupenda pia.

Kweli wanivumilia, mwingine ‘ngeshakimbia,
Hatiya najisikia, haya nayokufanyia,
Sipendi ukiumia, ni mambo yamezidia.

Si punde nitatulia, nawe utafurahia,
Machozi unayolia, kicheko kitakujia,
Mpenzi wangu tulia, kwako ningali na nia.

Bado nakufikiria, moyoni umenijaa,
Bado ninakuzimia, mwingine hajanifaa,
Unimulikie njia, kwangu uwe ndiye taa.

Upunguze kuumia, sipendi kukuchunia,
Basi uwache kulia, si punde nitatulia,
Mazuri twapigania, ndani ya hii dunia.

Thursday, June 3, 2010

Hepi bethidei Erik

Mtoto mzuri Erik,
Twamwoma Mungu akubariki,
Akulinde katika mikiki,
Ndani ya hii dunia.

Mungu akupe afya njema,
Akwepushie mbali homa,
Akubariki katika kusoma,
Akili zaidi kukujalia.

Akufanye mtoto mzuri,
Kwa wazazi uwe johari,
Nao wakwonee fahari,
Kama maua ukachanua.

Daima akujalie busara,
Ili usiwe nazo papara,
Wala mtu mwenye hasira,
Bali mwenye kutulia.

Uwe mtu mpatanishi,
Daima pawapo ubishi,
Jiepushe ulalamishi,
Dunia utaifurahia.

Ujaaliwe upendo tele,
Nyumbani nako shule,
Usiwatenge watu wale,
Wala kuwachukia.

Uwe mtu wa sala,
Hata kabla ya kulala,
Na wakati wako wa kula,
Uwaombee wenye njaa.

U kama jemedari,
Kwa wako umahiri,
Simama kwenye mstari,
Mungu atakusimamia.

Heri ya siku ya kuzaliwa,
Maisha marefu utapewa,
Daima unaombewa,
Na mema tunakutakia.

Wasalaam,
Anko Fadhy.