Sunday, May 23, 2010

Ukishikwa shikamana

Us'ende huko na huko,
Kwa machoyo mpauko,
Usitoboe mfuko,
Kesho ufanye tambiko,
Waitwe wasokuweko,
Wasadifu hoja zako,
Ukishikwa shikamana.

Kiraka ju'ye kiraka,
Kesho sipate wahka,
Mbuyu kuuzunguka,
Si dongo kufinyangika,
Awaye akakushika,
Kwae moyo kutunuka,
Ukishikwa shikamana.

Kutwa nzima barazani,
Keti weye jamvini,
Sera zino mdomoni,
Wajua ya duniani,
Uvivu uli kazini,
Wangoja letewa ndani,
Ukishikwa shikamana.

Maisha si tu safari,
Ni vita iso johari,
Ushindi u haradari,
Kushindwa siko fahari,
Kichwani hebu fikiri,
Kesho isiwe sifuri,
Ukishikwa shikamana.

Kama wangoja we ngoja,
Wataka uwe kiroja,
Uduvi havai koja,
Kwa utepetevu'wo mja,
Simama onesha haja,
Sibakiwe na mrija,
Ukishikwa shikamana.

Mgongoni wateleza,
Kutwa kucha wachagiza,
Wenzako wameyaweza,
Si filimbi kupuliza,
Bali mema kunuiza,
Hata usiku wa kiza,
Ukishikwa shikamana.

6 comments:

 1. ninunulie na supa gluuuuuuuu mweeeeeeeeee mtani unanikuna kisogo kwa mistari bwana

  ReplyDelete
 2. ninanukuu "Maisha si tu safari,
  Ni vita iso johari,
  Ushindi u haradari,
  Kushindwa siko fahari,
  Kichwani hebu fikiri,
  Kesho isiwe sifuri,
  Ukishikwa shikamana"mwisho wa kunukuu:- kama kawaidi kila nikipita hapa huwa naburuika sana kwa kusoma mashairi yako mtani.

  ReplyDelete
 3. Mshairi hapa unatukumbusha kuweka juhudi kwa kila mema tuyafanyayo. Tusikate tamaa pale tunapokutana na changamoto mbalimbali. Zaidi, tujitume na tusiwe watu wa kungoja ngoja na kuahirisha matatizo, tukabiliane nayo kwa wakati muafaka. Hii ni kwa kadiri ya mimi nilivyoelewa maudhui ya shairi.

  Kaka, nijuze maana ya misamiati hii, uduvi, koja, wahka na haradari.
  Asante sana kaka.

  ReplyDelete
 4. Kaka Albert, ushairi ni maneno machache yenye kubeba maana pana. Tafsiri huweza kutofautiana baina ya mtu mmoja na mwingine.

  Nafurahi kukupa maana ya maneno kama ulivyohitaji.

  Uduvi-ni samaki jamii ya kamba wapatikanao baharini kwenye maji madogo sana. Nao ni wadogo sana.

  Koja-ni mtungo ama taji la maua avishwalo mtu apongezwapo. Huwa ni kama zawadi ama pambo.

  Wahka-hutamkwa pia wahaka, ni wasiwasi ama kiherehere cha moyo.

  Haradali-ni mbegu ndogo sana zenye manjano, ni chungu sana mdomoni.

  Maneno hayo yanakuongoza kupata concept nzima ya mstari husika.

  Karibu zaidi.

  ReplyDelete