Thursday, May 27, 2010

Subi Nukta

hatukuzaliwa naye tumbo moja
lakini tumekua naye pamoja
lakini siyo toka zamani sana
bali tangia tulipofahamiana naye
akawa mwenzetu.

ni mwenzetu kabisa kabisa
kwa kuwa yu mtu mwema sana
ana roho ya peke yake
pengine hakuna wa kumfananisha naye
ni kweli hana mfanowe
watu wote waelewa hivyo.

amekuwa sehemu ya jamii yetu
tena kwa muda mrefu sana
ni mwenzetu kabisa
aki ya Ngai kweli vile
ni mwenzetu kabisa kabisa
nasi twampenda sana mno
huyu mtu wetu.

ni mkweli mno
tena pasipo kuogopa mtu yeyote
yu mwenye kujiamini kabisa
kabisa nyingi sana tu.
daima ni mwenye kujitolea
msaada kwa wengine.

yeye si m jivuni
wala mwenye kujisikia
la hasha!
yeye ni mwenye kuwajali watu
wakubwa kwa watoto
mambumbumbu kwa waloelimika
maana ni mtu wa watu
nao watu wanampenda sana
kwa kuwa naye awapenda sana.

nasi sote twamwombea
heri, heri tupu maishani.Shairi hili ni maalumu kwa dada Subi. Sina maneno mengi ya kukuelezea. Tunathamini sana mchango wako. Wewe unaweza usijue ni namna gani yale uyafanyayo yanavyogusa maisha ya watu wengine. Kipepeo haujui uzuri wa rangi zake, bali viumbe wengine tumtazamao. Uwe na maisha marefu. Pamoja daima.

9 comments:

 1. Ni mzuri kwa sura, umbo na tabasamu,
  Ni mjuvi wa tamathali, ngeli na nahau,
  Sote twampenda, japo yuko mbali,
  Kwa utamaduni hayuko mbali, rastazo zampendeza,
  Akilicheza segere, utadhni si mchaga wa marangu,
  Kwa mdundiko ndo usiseme, hodari wa kujimwayamwaya,
  Hakika twajivunia, kuwa na dada huyu.


  KUMBE NA MIE NIMO........!

  ReplyDelete
 2. Maisara, wasiwasi wangu ni kuwa tayari ushanifunika. Nimeifurahia hiyo mistari yako. Upo juu dadaa.

  ReplyDelete
 3. Subi hizo ni sifa zako kabisa na unastahili haswaaa. Tupo Pamoja .

  ReplyDelete
 4. Wow Kaka.
  Yaani umeandika hili na "kumtekenya" Da Maisara kuja na "verse" nyingine.
  Na hapa ndipo ninapoiona RAHA ya ku-blogu. Unaandika kisha unafunzwa kitu toka kwa mtoa maoni. Na hili ndilo tunaloweza kuenzi na kujivunia.
  Asante kwako kwa kuonesha kuukubali mchango mnono wa Da Subi. Asante na karibu tena Da Maisara na kama kawa, Dada "mtembezi" Yasinta asante saaana
  NAWATHAMINI NYOTE

  ReplyDelete
 5. Nimeliona shairi hili, nikiwa kazini
  Nikajiuliza hivi hili, kweli la nini
  Nikasema nijidhili, kitako niketi chini
  Nimsome Fadhli, kwa yale alosaini.

  Mimi si mshairi, na ni ndoto nijitahidi kwani kuhariri siwezi ndiposa napaswa kutoa shukrani na kushukuru ndugu, jamaa na rafiki zangu Fadhili, Maisara na Yasinta kwa yote mliyoyaandika. Kama sikuwa najifahamu, nimepata kufahamu kupitia kwenu kwa haya mliyoyaandika kunihusu.

  Langu moja, naomba aliyeniwezesha kufanya hivi hata ninyi mkaona inafaa, basi asinipungukie ufahamu na KAMWE asiniruhusu kujivuna wala kujipiga kifua kwa kudhani nimekuwa kichwa hadi nijitape. Ndugu zangu mmekuwa pamoja nami, na ninarudia kusema sentensi ile ile, niyafanyayo ni kwa upendo na kutaka kujua, nami hupenda na kujivunia sana kuwaonesha wengine kile nilichokiona, hivyo kadiri ninavyopata changamoto, ndivyo ninavyozidi kutaka kuchokonoa zaidi ili nipate kipya zaidi nitoe zaidi - iko raha katika kutoa kuliko kupokea - ni raha zaidi kile unachotoa kikamfaa na mwingine.

  Nitashukuru namna gani kwa sifa hizi?
  Nitatoa shukrani na kuzirudisha kwake aliyeniwezesha.

  Sikuja hapa duniani kwa uwezo wangu, sikuwa nilivyo kwa uwezo wangu, hivyo aliyenileta duniani na kujigawia alichonigawia, sifa zote na shukrani hizi zimwendee Yeye, milele na milele.

  Ndugu zangu, Mbarikiwe sana!

  ReplyDelete
 6. Nilitaka KUMSHUKURU Da SUBI kwa shukrani zake. Na sababu kubwa ni hii sentensi "Sikuja hapa duniani kwa uwezo wangu, sikuwa nilivyo kwa uwezo wangu, hivyo aliyenileta duniani na kujigawia alichonigawia, sifa zote na shukrani hizi zimwendee Yeye, milele na milele."

  She knocked me out (again) kwa BUSARA alizonazo.

  ReplyDelete
 7. Kaka Mubelwa nami nimezisoma hizo shukrani za Da Subi kwa hisia za heshima na upendo. Da Subi amekuwa na kipaji kingine cha kutumia maneno yanayogusa.
  Labda niseme, ahsante sana da Subi, unastahili wingi wa sifa na shukrani kutoka kwetu.
  Masi twazidi kukuombea uwe hivi ulivyo siku zote.
  Shukrani zingine, nazileta kwenu wanablog makini wa kike. Jamii ya kublog ianyo sababu ya kujivunia uwepo wenu.

  ReplyDelete
 8. Subi umesema kweli kabisa nimepapenda hapa rafiki nawe huchoki kuchokonoa watu haya "Sikuja hapa duniani kwa uwezo wangu, sikuwa nilivyo kwa uwezo wangu, hivyo aliyenileta duniani na kujigawia alichonigawia, sifa zote na shukrani hizi zimwendee Yeye, milele na milele."
  Upendo Daima.

  ReplyDelete