Sunday, May 16, 2010

Nina hamu nawe

Usingizi siupati, kama wewe upo mbali,
Mawazo kila wakati, kwani kwako sina hali,
Siku moja haipiti, nimepatwa na muhali,
Kweli nina hamu nawe, fanya hima sichelewe.

Nilipo nakungojea, kwa mahaba na bashasha,
Tabibu ulobobea, homa yangu kuishusha,
Furaha kuniletea, maishani kunitosha,
Kweli nina hamu nawe, fanya hima sichelewe.

Pambo la mwangu moyoni, pekee kwenye dunia,
Chakula mwangu rohoni, hakuna wa kufikia,
Jichoni mwangu u mboni, wewe wanonyesha njia,
Kweli nina hamu nawe, fanya hima sichelewe.

Hata niwapo dhaifu, we wanifanya imara,
Maneno yangu sadikifu, hakika watia fora,
Nami s'achi kukusifu, hata mara hedashara,
Kweli nina hamu nawe, fanya hima sichelewe.

Nakungoja na sichoki, ni raha niwapo nawe,
Unipooze ashiki, juu yako ninogewe,
Kwingine sihangaiki, thamani i kwako wewe,
Kweli nina hamu nawe, fanya hima sichelewe.

Wanilisha nikashiba, bila ya choyo chochote,
Kwa penzi lako la huba, linifanyalo niote,
Umejawa na mahaba, nilikesha nikupate,
Kweli nina hamu nawe, fanya hima sichelewe.

3 comments:

 1. mtani huyu wifi inabidi afanye haraka kweli maana tumeshoka kusubiri kwani twataka aje na harusi iwe pia vifaranga tuvione. Shairi bambi kweli. Upendo daima!!

  ReplyDelete
 2. Mwambie kaka asijekuta umeshajitundika manake watu wa kusini kwa mihasira...lol!

  Nawe mdada, acha kujishaua...halahala muwahi jamaa limekuzimikiaga...yeeee!!!!

  ReplyDelete
 3. "Mwambie kaka asijekuta umeshajitundika manake watu wa kusini kwa mihasira...lol!"

  WATU WA KUSINI KWA MIHARIRA WEWE KAKA CHACHA UMEWAONA WAPI???

  ReplyDelete