Monday, May 3, 2010

Nani kairoga soka

Nimefikiria sana, bado jawabu sipati,
Naja kwenu waungwana, kwa staha yenye dhati,
Kwenu mnaoyaona, mseme huu wakati,
Nani kairoga soka, timu zaja zapotea.

Niiseme ligi kuu, ivumayo Tanzania,
Mbona hili jungu kuu, ukoko lauishia,
Lini uje unafuu, mikoa kufurahia?
Nani kairoga soka, timu zaja zapotea.

Miaka yenda yarudi, bado ni Simba na Yanga,
Zingine vipi juhudi, timu hizi kuzifunga,
Ama zifukizwe udi, zikakeshe kwa mganga,
Nani kairoga soka, timu zaja zapotea.

Ilikuwapo Milambo, timu ile ya Tabora,
Kweli ilifanya mambo, kama Bandari Mtwara,
Mambo yamekwenda kombo, nazo zimeshadorora,
Nani kairoga soka, timu zaja zapotea.

Wapi Tukuyu Stars, ilishinda Tanzania,
Siku hizi haijiwezi, Kaka aliiachia,
Imeshuka zote ngazi, imebakia historia,
Nani kairoga soka, timu zaja zapotea.

Kuna Reli toka Moro, kiboko yake vigogo,
Haikuwa uchochoro, iliachia vipigo,
Sasa imekwenda doro, mithili ya mfu mbogo,
Nani kairoga soka, timu zaja zapotea.

Tanga Coastal Union, na African Sport,
Soka lake uwanjani, lilikuwa kwenye chati,
Sote tulilitamani, sasa zote zi kaputi,
Nani kairoga soka, timu zaja zapotea.

Nazareth na Lipuli, timu kutoka Iringa,
Zenye soka la ukweli, wananchi wakaringa,
Zimepigwa jini kali, zote sasa zaboronga,
Nani kairoga soka, timu zaja zapotea.

Pilsner na Sigara, Pan na Nyota Nyekundu,
Dar ilikuwa imara, kwa soka lenye utundu,
Timu zikawa vinara, zimekwisha kama bandu,
Nani kairoga soka, timu zaja zapotea.

Timu ya Reli Kigoma, ama Ujenzi ya Rukwa,
CDA ya Dodoma, pia na Mji Mpwapwa,
Na Tiger ya Tunduma, zote zabaki kumbukwa,
Nani kairoga soka, timu zaja zapotea.

Ushirika toka Moshi, na Kariakoo Lindi,
Zilileta kashikashi, sasa soka haiendi,
Sasa ni ubabaishi, zimezama kwenye lindi,
Nani kairoga soka, timu zaja zapotea.

Singida hakuna tena, kama ilivyo Arusha,
Pamba ya Mwanza hakuna, iliwahi tetemesha,
Ni bora tukakazana, timu tukazirejesha,
Nani kairoga soka, timu zaja zapotea.

Ona Prisons Mbeya, daraja imeshashuka,
Yaongozwa sera mbaya, pasipo kujali hoja,
Wananchi wakagwaya, wakaona ya wasoja,
Nani kairoga soka, timu zaja zapotea.

Zipo na zingine nyingi, ambazo zimepotea,
Kisa uhaba shilingi, uongozi kugombea,
Malumbano ndo msingi, timu zinatokomea.
Nani kairoga soka, timu zaja zapotea.

Wananchi twahusika, soka Ulaya twapenda,
Nyumbani kunabomoka, ladidimia kandanda,
Tunapaswa kushituka, timu zetu kuzilinda,
Nani kairoga soka, timu zaja zapotea.


Serikali za mikoa, macho zapaswa fumbua,
Na wadau kujitoa, timu tukazifufua,
Ubovu kuuondoa, ambao soka waua,
Nani kairoga soka, timu zaja zapotea.

Wito kwenu shirikisho, mwache ubabaishaji,
Mambo mengine michosho, mwawakera wachezaji,
Soka la leo na kesho, lataka uwekezaji,
Nani kairoga soka, timu zaja zapotea.

Kaditama namaliza, kalamu naweka chini,
Soka kuitelekeza, hakika umajinuni,
Ni wajibu kuzikuza, timu zetu mikoani,
Nani kairoga soka, timu zaja zapotea.

2 comments:

 1. nice one, this is! aliyeuta soka letu ni Super Sport na binamu zake. Siku hizi utasikia "Sisi Man" au "Sisi Chelsea" sasa katika maisha kama haya unataraji soka letu liendelee vipi. wazungu ziku hizi hawatutawali phisically au harshly kama zamani. wanatutawala remotedly and mentaly. Vyao bora, vyetu duni.

  Zamani hapa mbeya kulikuwa na watu kama akina marehemu Kifamba. hawa waliweza kuchangia timu ya yanga kutoka mifukoni. sidhani kama kifamba aliweza kuchangia yanga ya dar, angeshindwa kuchangia tukuyu stars ambayo ndio ilikuwa ikiileta yanga.

  zamani pia yanga ikija mbeya (samahani naijua zaid yanga, hiyo ya kwenu siijui sana), watu walijitokeza kuwafanyia jambo jema lolote kadri ya uwezo wao. mathalani wasiokuwa na uwezo waliweza hata kuchangia nguvu zao katika kumenya viazi na kufua nguo.

  kilichotawala maendeleo ya soka 'enzi za mwalimu' kilikuwa mapenzi ya dhati yaliyoweza kuwafanya watu wajitoe kwa hali na mali.

  ReplyDelete
 2. Kaka ahsante sana kwa mchango wako. Maana umeongea jambo la msingi sana.

  Hiyo Yanga yako iliufaidi sana huu uzalendo.

  Hakika nasikitishwa sana na vifo hivi vibudu vya soka la mikoani. Hata hapa Dar timu hata za juzi Vijana Ilala, Ashanti Utd, Msimbazi Rovers zimefuata njia ya Pan na Nyota Nyekundu.

  ReplyDelete