Monday, May 31, 2010

Mapenzi halisi

Katika hadithi zile za kale,
Watu walipendana nyakati zile,
Kwa mapenzi matamu yenye ukweli,
Mapenzi yao hayakujali mali,
Mapenzi yao yalipendeza sana,
Mapenzi yao ya kuaminiana,
Mapenzi yale mie nayatamani,
Ninayahitaji kutoka moyoni,
Ninajuwa mapenzi hayachagui,
Yanapojenga moyo wenye uhai,
Kuna mioyo inajuwa kupenda,
Mapenzi yake hayawezi kupinda,
Mapenzi yawezayo kukuzuzuwa,
Mapenzi moyoni yaliyotulia,
Mapenzi halisi ninayoyaimba,
Ambayo kutoka kwako nayaomba.

Njoo sogea nipe pendo la dhati,
Mapenzi ya uwongo siyafuati,
Njoo kwangu mpenzi we usisite,
Nami nitakupa moyo wangu wote,
Nikisema hivi utanisikia,
Nikitaka hiki utanipatia,
Kumbuka siku ya kwanza nilisema,
Nakupenda wewe tu hadi kiama,
Nikaandika tungo kwa ajili yako,
Nikaonesha mapenzi yangu kwako,
Ndivyo hivyo kamwe sitobadilika,
Nitakupenda pasipo kukuchoka,
Mapenzi yangu kwako usiyakwepe,
Naomba mapenzi halisi unipe,
Kwangu wewe usiwe na wasiwasi,
Nami nitakupa mapenzi halisi.

2 comments:

 1. Mtani umenigusa kweli kweli ila punguza kunichoma mno Lol

  ReplyDelete
 2. Fadhy mpenzio nahisi anakusikia,
  Pia anakusubiri iko siku mtaonana,
  Na ndipo utakapoamini haraka haraka haina baraka
  Kilio chako anasikia na ahisi siku yake atakujibu nawe utafurahi
  Na mtapeana mapenzi halisi.
  Kila la kheri.

  ReplyDelete