Wednesday, May 26, 2010

Giza

Usiku uingiapo, kwenye uso wa dunia,
Nuru itokomeapo, mambo mengi hutokea,
Mchana yasingewepo, usiku husubiria,
Giza linaficha mengi, usiku una mamboye.

Mchana watakatifu, ngoja giza liingie,
Hufanya yalo mchafu, ni bora usisikie,
Wale 'ngewapa turufu, wala usiwapimie,
Giza linaficha mengi, usiku una mamboye.

Usiku ni makahaba, wala huwezi amini,
Wenye uzuri si haba, ambao 'ngewatamani,
Warembo wenye kushiba, usiku barabarani,
Giza linaficha mengi, usiku una mamboye.

Braza wa uhakika, hakosi tai shingoni,
Tena wa kuheshimika, nyumbani na kanisani,
Kumbe yeye ni kibaka, akaba watu njiani,
Giza linaficha mengi, usiku una mamboye.

Tunomwamini sana, hishma tele kumpa,
Kumbe ndo mshirikina, kwa tunguli nazo chupa,
Usoni alama hana, ni vigumu kumkwepa,
Giza linaficha mengi, usiku una mamboye.

Wapenda njia za panya, hulipenda sana giza,
Wengine kuwadanganya, kwa hila na kuchagiza,
Kwa njama waweze penya, wengine kuwapoteza,
Giza linaficha mengi, usiku una mamboye.

No comments:

Post a Comment