Monday, May 31, 2010

Mapenzi halisi

Katika hadithi zile za kale,
Watu walipendana nyakati zile,
Kwa mapenzi matamu yenye ukweli,
Mapenzi yao hayakujali mali,
Mapenzi yao yalipendeza sana,
Mapenzi yao ya kuaminiana,
Mapenzi yale mie nayatamani,
Ninayahitaji kutoka moyoni,
Ninajuwa mapenzi hayachagui,
Yanapojenga moyo wenye uhai,
Kuna mioyo inajuwa kupenda,
Mapenzi yake hayawezi kupinda,
Mapenzi yawezayo kukuzuzuwa,
Mapenzi moyoni yaliyotulia,
Mapenzi halisi ninayoyaimba,
Ambayo kutoka kwako nayaomba.

Njoo sogea nipe pendo la dhati,
Mapenzi ya uwongo siyafuati,
Njoo kwangu mpenzi we usisite,
Nami nitakupa moyo wangu wote,
Nikisema hivi utanisikia,
Nikitaka hiki utanipatia,
Kumbuka siku ya kwanza nilisema,
Nakupenda wewe tu hadi kiama,
Nikaandika tungo kwa ajili yako,
Nikaonesha mapenzi yangu kwako,
Ndivyo hivyo kamwe sitobadilika,
Nitakupenda pasipo kukuchoka,
Mapenzi yangu kwako usiyakwepe,
Naomba mapenzi halisi unipe,
Kwangu wewe usiwe na wasiwasi,
Nami nitakupa mapenzi halisi.

Thursday, May 27, 2010

Subi Nukta

hatukuzaliwa naye tumbo moja
lakini tumekua naye pamoja
lakini siyo toka zamani sana
bali tangia tulipofahamiana naye
akawa mwenzetu.

ni mwenzetu kabisa kabisa
kwa kuwa yu mtu mwema sana
ana roho ya peke yake
pengine hakuna wa kumfananisha naye
ni kweli hana mfanowe
watu wote waelewa hivyo.

amekuwa sehemu ya jamii yetu
tena kwa muda mrefu sana
ni mwenzetu kabisa
aki ya Ngai kweli vile
ni mwenzetu kabisa kabisa
nasi twampenda sana mno
huyu mtu wetu.

ni mkweli mno
tena pasipo kuogopa mtu yeyote
yu mwenye kujiamini kabisa
kabisa nyingi sana tu.
daima ni mwenye kujitolea
msaada kwa wengine.

yeye si m jivuni
wala mwenye kujisikia
la hasha!
yeye ni mwenye kuwajali watu
wakubwa kwa watoto
mambumbumbu kwa waloelimika
maana ni mtu wa watu
nao watu wanampenda sana
kwa kuwa naye awapenda sana.

nasi sote twamwombea
heri, heri tupu maishani.Shairi hili ni maalumu kwa dada Subi. Sina maneno mengi ya kukuelezea. Tunathamini sana mchango wako. Wewe unaweza usijue ni namna gani yale uyafanyayo yanavyogusa maisha ya watu wengine. Kipepeo haujui uzuri wa rangi zake, bali viumbe wengine tumtazamao. Uwe na maisha marefu. Pamoja daima.

Wednesday, May 26, 2010

Giza

Usiku uingiapo, kwenye uso wa dunia,
Nuru itokomeapo, mambo mengi hutokea,
Mchana yasingewepo, usiku husubiria,
Giza linaficha mengi, usiku una mamboye.

Mchana watakatifu, ngoja giza liingie,
Hufanya yalo mchafu, ni bora usisikie,
Wale 'ngewapa turufu, wala usiwapimie,
Giza linaficha mengi, usiku una mamboye.

Usiku ni makahaba, wala huwezi amini,
Wenye uzuri si haba, ambao 'ngewatamani,
Warembo wenye kushiba, usiku barabarani,
Giza linaficha mengi, usiku una mamboye.

Braza wa uhakika, hakosi tai shingoni,
Tena wa kuheshimika, nyumbani na kanisani,
Kumbe yeye ni kibaka, akaba watu njiani,
Giza linaficha mengi, usiku una mamboye.

Tunomwamini sana, hishma tele kumpa,
Kumbe ndo mshirikina, kwa tunguli nazo chupa,
Usoni alama hana, ni vigumu kumkwepa,
Giza linaficha mengi, usiku una mamboye.

Wapenda njia za panya, hulipenda sana giza,
Wengine kuwadanganya, kwa hila na kuchagiza,
Kwa njama waweze penya, wengine kuwapoteza,
Giza linaficha mengi, usiku una mamboye.

Sunday, May 23, 2010

Ukishikwa shikamana

Us'ende huko na huko,
Kwa machoyo mpauko,
Usitoboe mfuko,
Kesho ufanye tambiko,
Waitwe wasokuweko,
Wasadifu hoja zako,
Ukishikwa shikamana.

Kiraka ju'ye kiraka,
Kesho sipate wahka,
Mbuyu kuuzunguka,
Si dongo kufinyangika,
Awaye akakushika,
Kwae moyo kutunuka,
Ukishikwa shikamana.

Kutwa nzima barazani,
Keti weye jamvini,
Sera zino mdomoni,
Wajua ya duniani,
Uvivu uli kazini,
Wangoja letewa ndani,
Ukishikwa shikamana.

Maisha si tu safari,
Ni vita iso johari,
Ushindi u haradari,
Kushindwa siko fahari,
Kichwani hebu fikiri,
Kesho isiwe sifuri,
Ukishikwa shikamana.

Kama wangoja we ngoja,
Wataka uwe kiroja,
Uduvi havai koja,
Kwa utepetevu'wo mja,
Simama onesha haja,
Sibakiwe na mrija,
Ukishikwa shikamana.

Mgongoni wateleza,
Kutwa kucha wachagiza,
Wenzako wameyaweza,
Si filimbi kupuliza,
Bali mema kunuiza,
Hata usiku wa kiza,
Ukishikwa shikamana.

Sunday, May 16, 2010

Nina hamu nawe

Usingizi siupati, kama wewe upo mbali,
Mawazo kila wakati, kwani kwako sina hali,
Siku moja haipiti, nimepatwa na muhali,
Kweli nina hamu nawe, fanya hima sichelewe.

Nilipo nakungojea, kwa mahaba na bashasha,
Tabibu ulobobea, homa yangu kuishusha,
Furaha kuniletea, maishani kunitosha,
Kweli nina hamu nawe, fanya hima sichelewe.

Pambo la mwangu moyoni, pekee kwenye dunia,
Chakula mwangu rohoni, hakuna wa kufikia,
Jichoni mwangu u mboni, wewe wanonyesha njia,
Kweli nina hamu nawe, fanya hima sichelewe.

Hata niwapo dhaifu, we wanifanya imara,
Maneno yangu sadikifu, hakika watia fora,
Nami s'achi kukusifu, hata mara hedashara,
Kweli nina hamu nawe, fanya hima sichelewe.

Nakungoja na sichoki, ni raha niwapo nawe,
Unipooze ashiki, juu yako ninogewe,
Kwingine sihangaiki, thamani i kwako wewe,
Kweli nina hamu nawe, fanya hima sichelewe.

Wanilisha nikashiba, bila ya choyo chochote,
Kwa penzi lako la huba, linifanyalo niote,
Umejawa na mahaba, nilikesha nikupate,
Kweli nina hamu nawe, fanya hima sichelewe.

Tuesday, May 11, 2010

Chatu na siafu

Porini
Ndiyo kule msituni
Kwenye miti
Na udongo wenye rutuba.
Haiyumkini,
Mwenye mabavu,
Akataka,
Kuonesha yaliyo wazi,
Na kuficha
Yaliyofichwa,
Pengine.

Mabavu,
Wala si hoja,
Mradi maarifa.

Wewe useme,
Sema tu.
Mdomo unao,
Wastara.
Jitutumue,
Haswaa,
Maguvu unayo,
Waama.

Wao waseme,
Watasema tu,
Sauti wanayo,
Waadhi.
Hawana maguvu.
Umoja wao
Ndiyo silaha yao,
Watashinda.

Maana ilisemwa,
Kale na sasa
Wema,
Hushinda uovu.

Monday, May 3, 2010

Nani kairoga soka

Nimefikiria sana, bado jawabu sipati,
Naja kwenu waungwana, kwa staha yenye dhati,
Kwenu mnaoyaona, mseme huu wakati,
Nani kairoga soka, timu zaja zapotea.

Niiseme ligi kuu, ivumayo Tanzania,
Mbona hili jungu kuu, ukoko lauishia,
Lini uje unafuu, mikoa kufurahia?
Nani kairoga soka, timu zaja zapotea.

Miaka yenda yarudi, bado ni Simba na Yanga,
Zingine vipi juhudi, timu hizi kuzifunga,
Ama zifukizwe udi, zikakeshe kwa mganga,
Nani kairoga soka, timu zaja zapotea.

Ilikuwapo Milambo, timu ile ya Tabora,
Kweli ilifanya mambo, kama Bandari Mtwara,
Mambo yamekwenda kombo, nazo zimeshadorora,
Nani kairoga soka, timu zaja zapotea.

Wapi Tukuyu Stars, ilishinda Tanzania,
Siku hizi haijiwezi, Kaka aliiachia,
Imeshuka zote ngazi, imebakia historia,
Nani kairoga soka, timu zaja zapotea.

Kuna Reli toka Moro, kiboko yake vigogo,
Haikuwa uchochoro, iliachia vipigo,
Sasa imekwenda doro, mithili ya mfu mbogo,
Nani kairoga soka, timu zaja zapotea.

Tanga Coastal Union, na African Sport,
Soka lake uwanjani, lilikuwa kwenye chati,
Sote tulilitamani, sasa zote zi kaputi,
Nani kairoga soka, timu zaja zapotea.

Nazareth na Lipuli, timu kutoka Iringa,
Zenye soka la ukweli, wananchi wakaringa,
Zimepigwa jini kali, zote sasa zaboronga,
Nani kairoga soka, timu zaja zapotea.

Pilsner na Sigara, Pan na Nyota Nyekundu,
Dar ilikuwa imara, kwa soka lenye utundu,
Timu zikawa vinara, zimekwisha kama bandu,
Nani kairoga soka, timu zaja zapotea.

Timu ya Reli Kigoma, ama Ujenzi ya Rukwa,
CDA ya Dodoma, pia na Mji Mpwapwa,
Na Tiger ya Tunduma, zote zabaki kumbukwa,
Nani kairoga soka, timu zaja zapotea.

Ushirika toka Moshi, na Kariakoo Lindi,
Zilileta kashikashi, sasa soka haiendi,
Sasa ni ubabaishi, zimezama kwenye lindi,
Nani kairoga soka, timu zaja zapotea.

Singida hakuna tena, kama ilivyo Arusha,
Pamba ya Mwanza hakuna, iliwahi tetemesha,
Ni bora tukakazana, timu tukazirejesha,
Nani kairoga soka, timu zaja zapotea.

Ona Prisons Mbeya, daraja imeshashuka,
Yaongozwa sera mbaya, pasipo kujali hoja,
Wananchi wakagwaya, wakaona ya wasoja,
Nani kairoga soka, timu zaja zapotea.

Zipo na zingine nyingi, ambazo zimepotea,
Kisa uhaba shilingi, uongozi kugombea,
Malumbano ndo msingi, timu zinatokomea.
Nani kairoga soka, timu zaja zapotea.

Wananchi twahusika, soka Ulaya twapenda,
Nyumbani kunabomoka, ladidimia kandanda,
Tunapaswa kushituka, timu zetu kuzilinda,
Nani kairoga soka, timu zaja zapotea.


Serikali za mikoa, macho zapaswa fumbua,
Na wadau kujitoa, timu tukazifufua,
Ubovu kuuondoa, ambao soka waua,
Nani kairoga soka, timu zaja zapotea.

Wito kwenu shirikisho, mwache ubabaishaji,
Mambo mengine michosho, mwawakera wachezaji,
Soka la leo na kesho, lataka uwekezaji,
Nani kairoga soka, timu zaja zapotea.

Kaditama namaliza, kalamu naweka chini,
Soka kuitelekeza, hakika umajinuni,
Ni wajibu kuzikuza, timu zetu mikoani,
Nani kairoga soka, timu zaja zapotea.