Monday, April 12, 2010

Mwanangu

Mwanangu uketi chini, mambo haya nikwambie,
Nisikie kwa makini, kichwani yazingatie,
Usiyaweke pembeni, kazi ukayafanyie,
Mwanangu hii dunia, yahitaji umakini.

Mwanangu wajuwe watu, uishi nao vizuri,
Jifunze kuwa na utu, utende kwa kufikiri,
Usiwadhulumu katu, wemawo uwe hiyari,
Mwanangu katende wema, usingoje shukrani.

Mwanangu wacha papara, wende mwendo taratibu,
Itangulize busara, hata panapo majibu,
Jisafishe yako sura, uepuke majaribu,
Nawe wonekane vema, uwe na yako staha.

Mwanangu wewe ukuwe, ili uje kuyaona,
Siyo majumba ya Kawe, ama jiji kubwa sana,
Bali ukayaelewe, maisha kila aina,
Yenye watu ndani yake, wenye vitu ndani yao.

Mwanangu si lelemama, maisha ni kupambana,
Kuna watu waso wema, kwa macho hutowaona,
Ikuze yako hekima, nayo ikuchunge sana,
Maana ndiyo silaha, dunia yajaa hila.

Mwanangu kuza imani, umtegemee Mungu,
Sidhulumu masikini, ukavunja chake chungu,
Uzidishe umakini, kwao hao walimwengu,
Dunia wala si mbaya, wabaya ni walimwengu.

Mwanangu ujihadhari, na vicheko midomoni,
Mioyoni si wazuri, wala usiwaamini,
Wajichimbia kaburi, wewe kufukiwa chini,
Marafiki wasaliti, ndivyo iwavyo daima.

Mwanangu hii dunia, imejaa uhadaa,
Mambo yakikunyokea, marafiki wanajaa,
Siku yakikuchachia, wote wanakukataa,
Kwao urafiki vitu, bilavyo hakuna pendo.

Mwanangu chunga kauli, pindi unapoongea,
Penda kusema ukweli, mema ukayatetea,
Uepuke ubatili, ubaya sije endea,
Mdomo ndio ubao, watu ndipo hukusoma.

Mwanangu nakushukuru, najua umesikia,
Ninakuombea nuru, Mola kukuangazia,
Mola atakunusuru, na mabaya ya dunia,
Mwanangu uishi vema, maisha kufurahia.Kila mzazi anapenda mwanawe awe na wakati mzuri maishani. Bado sina mtoto, lakini nimejaribu kuvaa uzazi na kuandika tungo hii. Naamini kila mzazi huwa anamfundisha mtoto wake namna bora ya kuishi na watu duniani. Shairi hili ni zawadi kwa wale wote ambao ni wazazi.

3 comments:

  1. nanukuu"Kila mzazi anapenda mwanawe awe na wakati mzuri maishani. Bado sina mtoto, lakini nimejaribu kuvaa uzazi na kuandika tungo hii. Naamini kila mzazi huwa anamfundisha mtoto wake namna bora ya kuishi na watu duniani. Shairi hili ni zawadi kwa wale wote ambao ni wazazi." mwisho wa kunukuu:- Asante sana kwa zawadi hii nzuri nimeriprint na kuwasomea wanangu na nitakuwa nawasomea kila wakati ili kuwakumbusha na ninaamini utakuwa baba/ mzazi,mlezi mmoja mzuri sana kaka Fadhy. Na ninakuombea umpate mwenza wako na mjaliwe kuppata matunda mema. Upendo Daima.

    ReplyDelete
  2. Ahsanteni sana da Yasinta na Kardinali Ng'wanambiti kwa kulipenda shairi hili. Kwa kuwa ninyi ni wazazi, naamini mmevutiwa nalo kiasi kikubwa.

    Pia niwatakieni wikendi njema.

    ReplyDelete