Saturday, April 24, 2010

Keti

Nyumbani kwangu karibu,
Nahisi jambo limekusibu,
Chukua kiti nisogee karibu,
Unieleze mambo taratibu,
Nina hamu ya kusikia.

Sema yote pasipo kuogopa,
Uaminifu wa kweli nakupa,
Nje siri siwezi kuzitupa,
Sema pasipo neno kulikwepa,
Usiogope mambo ya dunia.

Wasema umetendewa jambo baya,
Na mtu wa karibia yako kaya,
Wala usimwombe duwa mbaya,
Mwombee yeye aepushwe mabaya,
Nawe Mola atakubarikia.

Nyamaza basi wacha kulia,
Kwangu maumivu wayachochea,
Lolote baya walilokutendea,
Huna haja ya kuwahesabia,
Bali duwa njema kuwaombea.

Huna haja tena ya kuumia,
Madhali hayo yamekwishatokea,
Vema maisha ya mbele kuyaangalia,
Hao wengine hawatokusaidia,
Zaidi ya majungu kukujengea.

1 comment:

 1. nakaribia nakaribia,
  ili niweze kukueleza lilnalonisibu
  Je? hunioni nimekaa hapa karibu nawe?
  na taratibu nakueleza
  huku nimekuegemea kifuani.

  ReplyDelete