Tuesday, April 27, 2010

Wewe tu

Mpenzi wangu sikia,
Maneno ninayokwambia,
Kwamba nakupenda,
Wewe.
Nitakuja hadi kwenu,
Niwaone wazazi wako,
Niwaambie nakupenda,
Wewe.

Niahidi utanipenda,
Siku zote maishani,
Kwa kuwa nakupenda,
Wewe.
Kwangu hakuna mwingine,
Nitayempenda zaidi,
Niamini nakupenda,
Wewe.

Najisikia fahari,
Ninapopendana nawe,
Nitazidi kukupenda,
Wewe.
Sogea karibu nami,
Nilipate pendo lako,
Nizidishe kukupenda,
Wewe.


Nililiandika shairi hili nikiwa kidato cha tano pale Mkwawa High School. Nimeona si vibaya nikiliweka jamvini hapa.

Saturday, April 24, 2010

Keti

Nyumbani kwangu karibu,
Nahisi jambo limekusibu,
Chukua kiti nisogee karibu,
Unieleze mambo taratibu,
Nina hamu ya kusikia.

Sema yote pasipo kuogopa,
Uaminifu wa kweli nakupa,
Nje siri siwezi kuzitupa,
Sema pasipo neno kulikwepa,
Usiogope mambo ya dunia.

Wasema umetendewa jambo baya,
Na mtu wa karibia yako kaya,
Wala usimwombe duwa mbaya,
Mwombee yeye aepushwe mabaya,
Nawe Mola atakubarikia.

Nyamaza basi wacha kulia,
Kwangu maumivu wayachochea,
Lolote baya walilokutendea,
Huna haja ya kuwahesabia,
Bali duwa njema kuwaombea.

Huna haja tena ya kuumia,
Madhali hayo yamekwishatokea,
Vema maisha ya mbele kuyaangalia,
Hao wengine hawatokusaidia,
Zaidi ya majungu kukujengea.

Monday, April 19, 2010

Wakati

Wahenga ati walisema
Wakati,
Ni ukuta.
Wahenga hawa
Walijawa busara.

Ati wakaongeza,
Kuwa
Mpiga ngumi ukuta,
Huumiza
Mkonowe.

Aisee!

Nani awezaye
Rusha yake ngumi?
Ukutani,
Akabaki salama.
Atoke wapi?

Monday, April 12, 2010

Mwanangu

Mwanangu uketi chini, mambo haya nikwambie,
Nisikie kwa makini, kichwani yazingatie,
Usiyaweke pembeni, kazi ukayafanyie,
Mwanangu hii dunia, yahitaji umakini.

Mwanangu wajuwe watu, uishi nao vizuri,
Jifunze kuwa na utu, utende kwa kufikiri,
Usiwadhulumu katu, wemawo uwe hiyari,
Mwanangu katende wema, usingoje shukrani.

Mwanangu wacha papara, wende mwendo taratibu,
Itangulize busara, hata panapo majibu,
Jisafishe yako sura, uepuke majaribu,
Nawe wonekane vema, uwe na yako staha.

Mwanangu wewe ukuwe, ili uje kuyaona,
Siyo majumba ya Kawe, ama jiji kubwa sana,
Bali ukayaelewe, maisha kila aina,
Yenye watu ndani yake, wenye vitu ndani yao.

Mwanangu si lelemama, maisha ni kupambana,
Kuna watu waso wema, kwa macho hutowaona,
Ikuze yako hekima, nayo ikuchunge sana,
Maana ndiyo silaha, dunia yajaa hila.

Mwanangu kuza imani, umtegemee Mungu,
Sidhulumu masikini, ukavunja chake chungu,
Uzidishe umakini, kwao hao walimwengu,
Dunia wala si mbaya, wabaya ni walimwengu.

Mwanangu ujihadhari, na vicheko midomoni,
Mioyoni si wazuri, wala usiwaamini,
Wajichimbia kaburi, wewe kufukiwa chini,
Marafiki wasaliti, ndivyo iwavyo daima.

Mwanangu hii dunia, imejaa uhadaa,
Mambo yakikunyokea, marafiki wanajaa,
Siku yakikuchachia, wote wanakukataa,
Kwao urafiki vitu, bilavyo hakuna pendo.

Mwanangu chunga kauli, pindi unapoongea,
Penda kusema ukweli, mema ukayatetea,
Uepuke ubatili, ubaya sije endea,
Mdomo ndio ubao, watu ndipo hukusoma.

Mwanangu nakushukuru, najua umesikia,
Ninakuombea nuru, Mola kukuangazia,
Mola atakunusuru, na mabaya ya dunia,
Mwanangu uishi vema, maisha kufurahia.Kila mzazi anapenda mwanawe awe na wakati mzuri maishani. Bado sina mtoto, lakini nimejaribu kuvaa uzazi na kuandika tungo hii. Naamini kila mzazi huwa anamfundisha mtoto wake namna bora ya kuishi na watu duniani. Shairi hili ni zawadi kwa wale wote ambao ni wazazi.