Monday, March 8, 2010

Wanawake mnaweza

Nami leo ninasema, juu yenu wanawake,
Ninyi kwetu ndio mama, shukurani ziwafike,
Hakika mu watu wema, sina budi niandike,
Wanawake mnaweza, zidini kuwa imara.

Hapo kale mlitengwa, tukidhani hamtoweza,
Pande zote mkapingwa, mfumo kuendekeza,
Ubosi hamkupangwa, watu wakawachagiza,
Wanawake mnaweza, zidini kuwa imara.

Dunia yabadilika, nanyi mkadhihirisha,
Mnayo nguvu hakika, mambo kuyasababisha,
Madaraka mkishika, kamwe hamwezi chemsha,
Wanawake mnaweza, zidini kuwa imara.

Ninyi ni walezi bora, kuanzia familia,
Mwaitumia busara, nayo maarifa pia,
Kamwe hamna papara, malengo kuyafikia,
Wanawake mnaweza, zidini kuwa imara.

Mlio madaktari, pamoja na wauguzi,
Hakika mpo mahiri, kwa huo wenu ujuzi,
Kwenu na iwe fahari, kila mfanyapo kazi,
Wanawake mnaweza, zidini kuwa imara.

Mlio wanasheria, fani mmeibobea,
Haki kwa watu mwatoa, kwenu wanokimbilia,
Vipaji mwavitumia, jamii kusaidia,
Wanawake mnaweza, zidini kuwa imara.

Waandishi wa habari, mahiri kwenye sanaa,
Mwayaandika mazuri, kwa jamii yanofaa,
Werevu wa kufikiri, na hekima ilojaa,
Wanawake mnaweza, zidini kuwa imara.

Enyi mlio walimu, mwasaidia dunia,
Muitoapo elimu, jamii kuifikia,
Kazi ya kitaalamu, twapaswa kuwasifia,
Wanawake mnaweza, zidini kuwa imara.

Wanawake migodini, mwapambana na maisha,
Myasakapo madini, ufukara kukomesha,
Ingawa mu hatarini, bado mwajishughulisha,
Wanawake mnaweza, zidini kuwa imara.

Mfanyao biashara, ili uchumi kukuza,
Wanawake mnang'ara, hakika mnayaweza,
Daima mwatia fora, nami ninawapongeza,
Wanawake mnaweza, zidini kuwa imara.

Wanawake majumbani, nanyi nawapeni sifa,
Walezi wenye imani, wenye mengi maarifa,
Ninyi ni watu makini, wenye kuziziba nyufa,
Wanawake mnaweza, zidini kuwa imara.

Wanawake viongozi, msizipoteze dira,
Werevu uelekezi, zidini kuwa minara,
Dunia itawaenzi, furaha kwayo hadhira,
Wanawake mnaweza, zidini kuwa imara.

Mlio bado shuleni, zidini kukaza mwendo,
Mjitume darasani, kwa mema yenu matendo,
Msizame mitegoni, njia yenu iwe pindo,
Wanawake mnaweza, zidini kuwa imara.

Wanawake wote hoye, shangwe ulimwengu wote,
Mungu wetu atoaye, awapeni mema yote,
Yote awabarikiye, yalo mazuri mpate,
Wanawake mnaweza, zidini kuwa imara.

4 comments:

 1. Kaka Fadhy umesema yote kwa kweli ni jambo kujivuna sana nadhani wote tunajua ya kwamba bila mwanamke basi hakuna ukamilifu. Ahsante sana kwa shairi hili nimeprint nitahifadhi kama ukumbusho. Wnawake wote hoyeeeeeee!!!

  ReplyDelete
 2. Na iwe kumbukumbu kwa wanawake wote. Nimeandika shairi hili kwa ajili yenu. Da Yasinta we lichukue tu bila hofu.

  ReplyDelete
 3. mkwe shukrani kwa kuyatambua hayo

  ReplyDelete
 4. Ahsante sana mamamkwe wangu. Hakika nami natambua mnaweza. Heshima kwako. Uwe na wikendi njema.

  ReplyDelete