Sunday, March 28, 2010

Upo wapi niambie

Upo wapi niambie, maana mi siuoni,
Nataka nikusikie, nijue wasema nini,
Nenolo liniingie, likae mwangu moyoni,
Upo wapi niambie, ule urafiki wetu?

Rafiki uliahidi, siku zile za zamani,
Utaifanza juhudi, kamwe nisiende chini,
Ukasema wewe gadi, nisihofie moyoni,
Upo wapi niambie, ule urafiki wetu?

Rafiki nayakumbuka, manenoyo mdomoni,
Hakika niliridhika, nami nikakuamini,
Kwako hayakufichika, hata yale ya moyoni,
Upo wapi niambie, ule urafiki wetu?

Langu neno nikakupa, kwani nilikuthamini,
Sikuwahi kukukwepa, pindi uwapo shidani,
Gharama nilizilipa, ukosapo mfukoni,
Upo wapi niambie, ule urafiki wetu?

Nilikushika mkono, sikukuacha njiani,
Hukutengwa kwenye chano, ukapata cha kinywani,
Nikakupenda kwa hino, na kwa sala kwa Manani,
Upo wapi niambie, ule urafiki wetu?

Mambo nayo kegeuka, chubwii hadi shimoni,
Makubwa yakanifika, nikazama taabuni,
Nahitaji kuokoka, mwokozi wala simwoni,
Upo wapi niambie, ule urafiki wetu?

Rafiki nakutafuta, mbona sasa sikuoni?
Kwa machozi nimetota, atayenifuta nani?
Mwenzako mie natweta, wewe upo kona gani?
Upo wapi niambie, ule urafiki wetu?

Rafiki wanikimbia, hata haya huioni,
Hutaki nisaidia, kumbe umo furahani,
Mabaya waniombea, nizidi zama shidani,
Upo wapi niambie, ule urafiki wetu?

Kupiga simu hutaki, ujuwe ni hali gani,
Kumbe wala hukumbuki, siku zetu za zamani,
Nilikufaa kwa dhiki, leo mie ni shetani,
Upo wapi niambie, ule urafiki wetu?

Rafiki wanitangaza, vibaya barabarani,
Kama we umemaliza, mambo yote duniani,
Wanisengenya wabeza, wapenda niende chini,
Upo wapi niambie, ule urafiki wetu?

Kama nimekukosea, niambie kitu gani,
Si hivi kunitendea, wakati nimo shidani,
Kwani ningetegemea, niwepo pako begani,
Upo wapi niambie, ule urafiki wetu?

Wewe ndiwe waniliza, kuliko nira shingoni,
Tena waniteketeza, kuliko moto porini,
Wajaribu nimaliza, sijui wapata nini,
Upo wapi niambie, ule urafiki wetu?

Msumari wapigia, palepale kidondani,
Wajua ninaumia, wataka wone siponi,
Nawe unafurahia, kwani waishi mbinguni,
Upo wapi niambie, ule urafiki wetu?

Nazidi kumwomba Mungu, moyoni nina amani,
Na wewe rafiki yangu, nakukumbuka salani,
Nimejua malimwengu, bado nipo safarini,
Upo wapi niambie, ule urafiki wetu?


Ni simulizi ya kweli, inihusuyo mimi mwenyewe.
Namshukuru Mungu kwa kila jambo.

3 comments:

 1. Tenda wema nenda zako,Mungu yupo nawe mtani. Nimerudia mara tatu kusoma hili shairi na kujikuta nadondosha chozi Duniani hapa. Upendo Daima

  ReplyDelete
 2. Upo wapi mwambie,Fadhy apate tulia,
  wafanya kaka alie,moyoni anaumia,
  u wapi upendwae,Fadhy apate tulia,
  haraka umrudie,upo wapi akwambia.

  ReplyDelete
 3. Ahsante sana da Yasinta na kaka Albert. Nililiandika shairi hili nikiwa na hisia kali. Nilishindwa kujizuia machozi. Lakini nilipomaliza kuandika, nikajihisi nimetua mzigo. Nawashukuruni kwa kunipokea mzigo huo.
  Kama nikivyosema, ni habari ya kweli kabisa kabisa.
  Nina mtu niliyedhani ni rafiki, nikajitoa kwake kwa moyo wangu wote, na kwa kila nilivyoweza.
  Mwenzangu akaja kuniletea matatizo makubwa sana. Na alipofanikiwa, akanipotezea mawasiliano kama hanijui vile.
  Kilikuwa kipindi kigumu sana kwangu. Kigumu kuliko chochote nachoweza kukikumbuka maishani.
  Nikapiga moyo konde. Ninamshukuru sana Mungu baada ya siku chache niliweza kurudi katika hali ya kawaida.
  Sasa nina amani na furaha moyoni. Nimepata somo muhimu sana maishani.
  Maisha yanaendelea.

  ReplyDelete