Friday, March 26, 2010

Safari yangu ina miaka mitatu

Najua nilipoanzia,
Sijui nitapoishia,
Najua napiga hatua,
Kwa sababu ninayo nia,
Hakika nimedhamiria,
Mbele nizidi kusogea.

Hadithi nayosimulia,
Ushairi nilikoanzia,
Zamani iliwahi kutokea,
Kutunga nilitamania,
Sikuacha mie kuwazia,
Lakini mbinu sikuzijua.

Siku mama nikamwendea,
Neno nikamwambia,
Yeye akanishangaa,
Mtoto wangu kweli una nia,
Akasema vina, mizani zingatia,
Ongeza maarifa pia.

Somo likaniingia,
Kalamu nikaichukua,
Mawazo niloyafikiria,
Ndiyo nikajiandikia,
Nami nikajigundua,
Hee! Mshairi nimekua.

Miaka yaenda yakimbia,
Nami nikadhamiria,
Wengine nataka kuwafikia,
Kiushairi kuwaambia,
Nani jama atanisaidia?

Ndesanjo akaja tokea,
Gazetini nikamfuatilia,
Akasema blog husaidia,
Ujumbe wengine kuwafikia,
Nikamsoma na kufurahia,
Neno lake nikalichukua.

Miaka mitatu ilotangulia,
Nami kigulu nayo njia,
Ufunguo nikaununua,
Blog niweze fungulia,
Hakika sikuwa natania,
Hapo nami nikazianzishia.

Nilianza sina naemjua,
Nilihisi upweke kunielemea,
Mungu akasema kijana tulia,
Taratibu marafiki utajipatia,
Nikaamini yale alonambia,
Nami nikazidi weka nia.

Mwaka ukawa wasogea,
Watu wanaanza nami kunijua,
Watu hawa wema nakwambia,
Asowajua kuna kitu ajikosea,
Nami huyo nikawazowea,
Nikawa nami kwenye familia,
Maisha yanazidi kusogea.

Sasa miaka mitatu imekimbia,
Bado mimi naifurahia,
Nataka nisiiache familia,
Maana nimeshaizowea,
Nao wenzangu wanifurahia,
Na ndiyo raha ya hii dunia,
Siyo mali kujijazia.

Hadithi nimesimulia,
Ahsanteni kunivumilia,
Wakati nahadithia,
Neno hili nawaambia,
Hakika nawafurahia,
Nazo shukrani kwenu natoa.

Safari inaendelea,
Njiani sitaki kuachia,
Siku Mola atakayonichukua,
Humu mwisho utafikia.

Pamoja daima.

1 comment:

  1. Hongera Diwani ya Fadhili kwa kutimiza miaka mitatu. Ni kweli ni safari ndefu imeifanya.
    Nikuambieni siri ambayo sasa sio siri tena ni kwamba haipiti siku bila kupitia ktk kibaraza hiki na kusoma mashairi kwani nimekuwa mdhaifu sana ya mashairi ya kibaraza hiki. HONGERA SANA.

    ReplyDelete