Monday, March 22, 2010

Leo miaka mitatu

Kwa jina lake Jalali, najawa furaha tele,
Tunapotoka ni mbali, twahitaji songa mbele,
Mungu yu kila mahali, milele yote milele,
Leo miaka mitatu, pale mwananchi mimi.

Nilianza ka utani, na miaka yasogea,
Jambo lile akilini, nilitaka kuongea,
Ningeshindwa asilani, kila mtu kumwendea,
Sasa miaka mitatu, sichoki na harakati.

Kublog siyo mchezo, bado sikati tamaa,
Bado naweka mkazo, blog zizidi kung'aa,
Na kuvishinda vikwazo, kwa mbio si kutambaa,
Ona miaka mitatu, ningali bado hewani,

Kublog kunayo raha, hakika naifaidi,
Kwa ari nayo madaha, nao wingi wa weledi,
Daima ipo furaha, siachi hilo kunadi,
Hii miaka mitatu, kwangu ni sawa na lulu.

Kuyasema bila woga, na wengine wasikie,
Zaweza kuwa ni soga, ujumbe uwaingie,
Baragumu kulipiga, sauti iwafikie,
Kwani miaka mitatu, bado safari ni ndefu.

Mwananchi na sichoki, nazidi kukaza buti,
Nitanena kwayo haki, kwa wote kila wakati,
Jamii itamalaki, kwazo zetu harakati,
Iwe miaka mitatu, chachu ya kusonga mbele.

Shime wajameni shime, jamii kuiamsha,
Tukazane tujitume, ujumbe kuufikisha,
Yafaayo tuyaseme, mabaya kurekebisha,
Mimi miaka mitatu, nitazidi kuwa nanyi.

Mimi mwananchi mimi!, ninasema ahsanteni,
Langu kamwe siwanyimi, kwani ninawapendeni,
Mpewe mengi makumi, baraka zake Manani,
Leo miaka mitatu, pale mwananchi mimi!

4 comments:

 1. Hongera sana blog ya MWANANCHI MIMI NA izidi kudumu. Hongera pia mtani Fadhy kwa kila ufanyacha .Upendo daima

  ReplyDelete
 2. Nakushukuru sana da Yasinta. Nakushukuru pia kwa kuwa nami wakati wote.
  Pamoja daima.

  ReplyDelete
 3. hii imetulia ni bonge la CV hilo kaka

  ReplyDelete
 4. Hongera MWANANCHI MIMI kwa kutimiza miaka mitatu!

  ReplyDelete