Tuesday, March 30, 2010

Amani

Amani hawi sokoni, auzwe kwa bei gani?
Afungwe kwa nailoni, nakishi atiwe ndani,
Bei yake bilioni, asimudu masikini,
Amani siyo maneno, amani huwa vitendo.

Siasa majukwaani, kutwa hubiri amani,
Kumbe mwao mioyoni, hata hawaithamini,
Wanayo ya mifukoni, mivundo yenye ubani,
Amani wanayo wao, wenye kuzitunga sera.

Amani kwa masikini, ipo tu mwake ndotoni,
Lakini si maishani, wakati hana thumuni,
Asoma magazetini, na sikio redioni,
Tamu za wanasiasa, maneno yenye kurembwa.

Sera zino vitabuni, mikakatiye pomoni,
Ila zao sizo kwani, parara zi midomoni,
Macho yeni heyoni, lila na fila zaani,
Kuhubiri wahubiri, ila matendo sifuri.

Sera za kijalalani, ama ubovu mtimani,
Hasi haiyumkini, ikatoke kundi gani,
Wote tukaibaini, ivishwe na kirauni,
Machozi yake amani, kwao hadi yakauke.

Chago chake anzuruni, urembo urujuani,
Chanzoche kili chamani, labda tuwe kijani,
Chama kile cha zamani, kichong'oa ukoloni,
Sasa siyo chetu tena, kipi kinacho amani?

Uchungu mwingi wa nini, amani kapewa nani?
Alofungia chumbani, tukose wa sebuleni,
Pengine sisi wageni, tuazime kwa jirani,
Yetu tunaifinyanga, kesho kilio kwa nani?

Kalamu naweka chini, wino upo ukingoni,
Amani usinihini, nikuweke kabatini,
Pambo wajapo wageni, wenyeji wone machoni,
Chako nje wasifia, nyumbani hakitumiki.


Nimeandika shairi hili kama maoni ya shairi Nakutafuta Amani (gonga kulisoma) lililoandikwa na kaka Albert Kissima na kuwekwa kibarazani kwake "Mwanamalenga"

4 comments:

 1. Ahsante sana kwa shairi hili zuri. Ama kweli najivunia kukufahamu kupitia blog na pia mashairi yako. Amani kwako mtani:-)

  ReplyDelete
 2. Amani bado jamani,ukweli muufahamu,
  kila siku redioni,ni madai ya walimu,
  wafanyakazi relini,wanyimwa haki muhimu,
  Kagera iko vitani,maisha huko magumu,
  kila siku ni kuhani,misiba ya walo tunu,
  nia yetu ni amani,daima inayodumu.

  Mengi Fadhy kayasema,machache niliyagusa,
  kaka nakupa heshima,pamoja tunasongesha.

  Heshima dada Yasinta,umoja ndio chereko,
  mchangowo twaupata,twajua uwepo wako.

  ReplyDelete
 3. Kaka Albert nakushukuru sana kwa kunipa idea ya shairi hili.

  Da Yasinta ahsante sana kwa kuipenda picha hii.

  ReplyDelete