Tuesday, March 30, 2010

Amani

Amani hawi sokoni, auzwe kwa bei gani?
Afungwe kwa nailoni, nakishi atiwe ndani,
Bei yake bilioni, asimudu masikini,
Amani siyo maneno, amani huwa vitendo.

Siasa majukwaani, kutwa hubiri amani,
Kumbe mwao mioyoni, hata hawaithamini,
Wanayo ya mifukoni, mivundo yenye ubani,
Amani wanayo wao, wenye kuzitunga sera.

Amani kwa masikini, ipo tu mwake ndotoni,
Lakini si maishani, wakati hana thumuni,
Asoma magazetini, na sikio redioni,
Tamu za wanasiasa, maneno yenye kurembwa.

Sera zino vitabuni, mikakatiye pomoni,
Ila zao sizo kwani, parara zi midomoni,
Macho yeni heyoni, lila na fila zaani,
Kuhubiri wahubiri, ila matendo sifuri.

Sera za kijalalani, ama ubovu mtimani,
Hasi haiyumkini, ikatoke kundi gani,
Wote tukaibaini, ivishwe na kirauni,
Machozi yake amani, kwao hadi yakauke.

Chago chake anzuruni, urembo urujuani,
Chanzoche kili chamani, labda tuwe kijani,
Chama kile cha zamani, kichong'oa ukoloni,
Sasa siyo chetu tena, kipi kinacho amani?

Uchungu mwingi wa nini, amani kapewa nani?
Alofungia chumbani, tukose wa sebuleni,
Pengine sisi wageni, tuazime kwa jirani,
Yetu tunaifinyanga, kesho kilio kwa nani?

Kalamu naweka chini, wino upo ukingoni,
Amani usinihini, nikuweke kabatini,
Pambo wajapo wageni, wenyeji wone machoni,
Chako nje wasifia, nyumbani hakitumiki.


Nimeandika shairi hili kama maoni ya shairi Nakutafuta Amani (gonga kulisoma) lililoandikwa na kaka Albert Kissima na kuwekwa kibarazani kwake "Mwanamalenga"

Sunday, March 28, 2010

Upo wapi niambie

Upo wapi niambie, maana mi siuoni,
Nataka nikusikie, nijue wasema nini,
Nenolo liniingie, likae mwangu moyoni,
Upo wapi niambie, ule urafiki wetu?

Rafiki uliahidi, siku zile za zamani,
Utaifanza juhudi, kamwe nisiende chini,
Ukasema wewe gadi, nisihofie moyoni,
Upo wapi niambie, ule urafiki wetu?

Rafiki nayakumbuka, manenoyo mdomoni,
Hakika niliridhika, nami nikakuamini,
Kwako hayakufichika, hata yale ya moyoni,
Upo wapi niambie, ule urafiki wetu?

Langu neno nikakupa, kwani nilikuthamini,
Sikuwahi kukukwepa, pindi uwapo shidani,
Gharama nilizilipa, ukosapo mfukoni,
Upo wapi niambie, ule urafiki wetu?

Nilikushika mkono, sikukuacha njiani,
Hukutengwa kwenye chano, ukapata cha kinywani,
Nikakupenda kwa hino, na kwa sala kwa Manani,
Upo wapi niambie, ule urafiki wetu?

Mambo nayo kegeuka, chubwii hadi shimoni,
Makubwa yakanifika, nikazama taabuni,
Nahitaji kuokoka, mwokozi wala simwoni,
Upo wapi niambie, ule urafiki wetu?

Rafiki nakutafuta, mbona sasa sikuoni?
Kwa machozi nimetota, atayenifuta nani?
Mwenzako mie natweta, wewe upo kona gani?
Upo wapi niambie, ule urafiki wetu?

Rafiki wanikimbia, hata haya huioni,
Hutaki nisaidia, kumbe umo furahani,
Mabaya waniombea, nizidi zama shidani,
Upo wapi niambie, ule urafiki wetu?

Kupiga simu hutaki, ujuwe ni hali gani,
Kumbe wala hukumbuki, siku zetu za zamani,
Nilikufaa kwa dhiki, leo mie ni shetani,
Upo wapi niambie, ule urafiki wetu?

Rafiki wanitangaza, vibaya barabarani,
Kama we umemaliza, mambo yote duniani,
Wanisengenya wabeza, wapenda niende chini,
Upo wapi niambie, ule urafiki wetu?

Kama nimekukosea, niambie kitu gani,
Si hivi kunitendea, wakati nimo shidani,
Kwani ningetegemea, niwepo pako begani,
Upo wapi niambie, ule urafiki wetu?

Wewe ndiwe waniliza, kuliko nira shingoni,
Tena waniteketeza, kuliko moto porini,
Wajaribu nimaliza, sijui wapata nini,
Upo wapi niambie, ule urafiki wetu?

Msumari wapigia, palepale kidondani,
Wajua ninaumia, wataka wone siponi,
Nawe unafurahia, kwani waishi mbinguni,
Upo wapi niambie, ule urafiki wetu?

Nazidi kumwomba Mungu, moyoni nina amani,
Na wewe rafiki yangu, nakukumbuka salani,
Nimejua malimwengu, bado nipo safarini,
Upo wapi niambie, ule urafiki wetu?


Ni simulizi ya kweli, inihusuyo mimi mwenyewe.
Namshukuru Mungu kwa kila jambo.

Friday, March 26, 2010

Safari yangu ina miaka mitatu

Najua nilipoanzia,
Sijui nitapoishia,
Najua napiga hatua,
Kwa sababu ninayo nia,
Hakika nimedhamiria,
Mbele nizidi kusogea.

Hadithi nayosimulia,
Ushairi nilikoanzia,
Zamani iliwahi kutokea,
Kutunga nilitamania,
Sikuacha mie kuwazia,
Lakini mbinu sikuzijua.

Siku mama nikamwendea,
Neno nikamwambia,
Yeye akanishangaa,
Mtoto wangu kweli una nia,
Akasema vina, mizani zingatia,
Ongeza maarifa pia.

Somo likaniingia,
Kalamu nikaichukua,
Mawazo niloyafikiria,
Ndiyo nikajiandikia,
Nami nikajigundua,
Hee! Mshairi nimekua.

Miaka yaenda yakimbia,
Nami nikadhamiria,
Wengine nataka kuwafikia,
Kiushairi kuwaambia,
Nani jama atanisaidia?

Ndesanjo akaja tokea,
Gazetini nikamfuatilia,
Akasema blog husaidia,
Ujumbe wengine kuwafikia,
Nikamsoma na kufurahia,
Neno lake nikalichukua.

Miaka mitatu ilotangulia,
Nami kigulu nayo njia,
Ufunguo nikaununua,
Blog niweze fungulia,
Hakika sikuwa natania,
Hapo nami nikazianzishia.

Nilianza sina naemjua,
Nilihisi upweke kunielemea,
Mungu akasema kijana tulia,
Taratibu marafiki utajipatia,
Nikaamini yale alonambia,
Nami nikazidi weka nia.

Mwaka ukawa wasogea,
Watu wanaanza nami kunijua,
Watu hawa wema nakwambia,
Asowajua kuna kitu ajikosea,
Nami huyo nikawazowea,
Nikawa nami kwenye familia,
Maisha yanazidi kusogea.

Sasa miaka mitatu imekimbia,
Bado mimi naifurahia,
Nataka nisiiache familia,
Maana nimeshaizowea,
Nao wenzangu wanifurahia,
Na ndiyo raha ya hii dunia,
Siyo mali kujijazia.

Hadithi nimesimulia,
Ahsanteni kunivumilia,
Wakati nahadithia,
Neno hili nawaambia,
Hakika nawafurahia,
Nazo shukrani kwenu natoa.

Safari inaendelea,
Njiani sitaki kuachia,
Siku Mola atakayonichukua,
Humu mwisho utafikia.

Pamoja daima.

Monday, March 22, 2010

Leo miaka mitatu

Kwa jina lake Jalali, najawa furaha tele,
Tunapotoka ni mbali, twahitaji songa mbele,
Mungu yu kila mahali, milele yote milele,
Leo miaka mitatu, pale mwananchi mimi.

Nilianza ka utani, na miaka yasogea,
Jambo lile akilini, nilitaka kuongea,
Ningeshindwa asilani, kila mtu kumwendea,
Sasa miaka mitatu, sichoki na harakati.

Kublog siyo mchezo, bado sikati tamaa,
Bado naweka mkazo, blog zizidi kung'aa,
Na kuvishinda vikwazo, kwa mbio si kutambaa,
Ona miaka mitatu, ningali bado hewani,

Kublog kunayo raha, hakika naifaidi,
Kwa ari nayo madaha, nao wingi wa weledi,
Daima ipo furaha, siachi hilo kunadi,
Hii miaka mitatu, kwangu ni sawa na lulu.

Kuyasema bila woga, na wengine wasikie,
Zaweza kuwa ni soga, ujumbe uwaingie,
Baragumu kulipiga, sauti iwafikie,
Kwani miaka mitatu, bado safari ni ndefu.

Mwananchi na sichoki, nazidi kukaza buti,
Nitanena kwayo haki, kwa wote kila wakati,
Jamii itamalaki, kwazo zetu harakati,
Iwe miaka mitatu, chachu ya kusonga mbele.

Shime wajameni shime, jamii kuiamsha,
Tukazane tujitume, ujumbe kuufikisha,
Yafaayo tuyaseme, mabaya kurekebisha,
Mimi miaka mitatu, nitazidi kuwa nanyi.

Mimi mwananchi mimi!, ninasema ahsanteni,
Langu kamwe siwanyimi, kwani ninawapendeni,
Mpewe mengi makumi, baraka zake Manani,
Leo miaka mitatu, pale mwananchi mimi!

Saturday, March 20, 2010

Kwenye mapambano

Vijana tusilale lale, lale,
Vijana tusilale lale, lale,
Kwenye mapambano,
Wote tuwe mshikamano,
Wote tushikane mikono,
Azimio letu liwe agano,
Tuwe na bora sera hino.

Tuwaamshe wale ili wasilale,
Tuyasafishe yote mabaya yale,
Tusingoje mtu alete somo,
Tuchangamke wote tuwemo,
Tusingoje yapite makamo,
Itatutesa sumu iliyomo,
Tusilale ndo uwe wetu msemo.

Kumekucha!

Tuesday, March 16, 2010

Maji ya mto

Huja,
Na kwenda zake,
Wala hayarudi tena.
Ati nini?
Iwavyo ndivyo,
Ilivyo!

Wala huwezi,
Asilani,
Abadani!
Kuyavuka,
Mara mbili.

Mh!
Wapi wewe?
Waweza dhani waweza.
Lakini kumbe,
Huwezi kamwe.

Yajapo,
Huenda zake.
Nawe ujapo,
Huyavuka maji yale.
Ukaenda zako!

Ukija tena,
Kuyavuka,
Wala si yale.
Bali,
Wavuka,
Maji mengine.

Maisha,
Ndiyo mkondo,
Yaendapo,
Yache yende zake.
Maana yapo.
Mengine,
Pengine huyajui.
Yalo,
Bora zaidi.

Jua lileeee!
Literemke.
Maji yaleeee,
Yenda zake!

Yapo,
Kumbe,
Mengine,
Yajayo.

Yenye kheri zaidi.

Thursday, March 11, 2010

Njoo nikwambie

Moyo wangu umenituma....
Hili neno nije kusema......
Moyo wahitaji kutuwama.....
Kwa moyowo ulo mwema.......
Moyo sasa unatamani......
Pendo lako la thamani.......
La pekee humu duniani......
Zawadi kutoka kwa Maanani......
Moyo wala hauna shaka.....
Kwani kwako umefika.....
Moyo wataka burudika.....
Kwa penzi lisomithilika.

Monday, March 8, 2010

Wanawake mnaweza

Nami leo ninasema, juu yenu wanawake,
Ninyi kwetu ndio mama, shukurani ziwafike,
Hakika mu watu wema, sina budi niandike,
Wanawake mnaweza, zidini kuwa imara.

Hapo kale mlitengwa, tukidhani hamtoweza,
Pande zote mkapingwa, mfumo kuendekeza,
Ubosi hamkupangwa, watu wakawachagiza,
Wanawake mnaweza, zidini kuwa imara.

Dunia yabadilika, nanyi mkadhihirisha,
Mnayo nguvu hakika, mambo kuyasababisha,
Madaraka mkishika, kamwe hamwezi chemsha,
Wanawake mnaweza, zidini kuwa imara.

Ninyi ni walezi bora, kuanzia familia,
Mwaitumia busara, nayo maarifa pia,
Kamwe hamna papara, malengo kuyafikia,
Wanawake mnaweza, zidini kuwa imara.

Mlio madaktari, pamoja na wauguzi,
Hakika mpo mahiri, kwa huo wenu ujuzi,
Kwenu na iwe fahari, kila mfanyapo kazi,
Wanawake mnaweza, zidini kuwa imara.

Mlio wanasheria, fani mmeibobea,
Haki kwa watu mwatoa, kwenu wanokimbilia,
Vipaji mwavitumia, jamii kusaidia,
Wanawake mnaweza, zidini kuwa imara.

Waandishi wa habari, mahiri kwenye sanaa,
Mwayaandika mazuri, kwa jamii yanofaa,
Werevu wa kufikiri, na hekima ilojaa,
Wanawake mnaweza, zidini kuwa imara.

Enyi mlio walimu, mwasaidia dunia,
Muitoapo elimu, jamii kuifikia,
Kazi ya kitaalamu, twapaswa kuwasifia,
Wanawake mnaweza, zidini kuwa imara.

Wanawake migodini, mwapambana na maisha,
Myasakapo madini, ufukara kukomesha,
Ingawa mu hatarini, bado mwajishughulisha,
Wanawake mnaweza, zidini kuwa imara.

Mfanyao biashara, ili uchumi kukuza,
Wanawake mnang'ara, hakika mnayaweza,
Daima mwatia fora, nami ninawapongeza,
Wanawake mnaweza, zidini kuwa imara.

Wanawake majumbani, nanyi nawapeni sifa,
Walezi wenye imani, wenye mengi maarifa,
Ninyi ni watu makini, wenye kuziziba nyufa,
Wanawake mnaweza, zidini kuwa imara.

Wanawake viongozi, msizipoteze dira,
Werevu uelekezi, zidini kuwa minara,
Dunia itawaenzi, furaha kwayo hadhira,
Wanawake mnaweza, zidini kuwa imara.

Mlio bado shuleni, zidini kukaza mwendo,
Mjitume darasani, kwa mema yenu matendo,
Msizame mitegoni, njia yenu iwe pindo,
Wanawake mnaweza, zidini kuwa imara.

Wanawake wote hoye, shangwe ulimwengu wote,
Mungu wetu atoaye, awapeni mema yote,
Yote awabarikiye, yalo mazuri mpate,
Wanawake mnaweza, zidini kuwa imara.