Thursday, February 11, 2010

Wasiwasi na Neno zuri

Humkosesha mtu raha, wasiwasi unakera,
Huleta nyingi karaha, hata kw'ongeza hasira,
Huwezi fanya madaha, wafungwa nayo nira,
Wasiwasi.

Wasiwasi ni utumwa, wa kuusumbua moyo,
Huleta kama kuumwa, yale yakusumbuayo,
Moyo wahisi kuchomwa, kwa yale yautesayo,
Wasiwasi.

Wasiwasi unaghasi, unakosesha amani,
Kutengwa unakuhisi, kama mwokozi humwoni,
Huharibu mitikasi, na kukurudisha chini,
Wasiwasi.

Neno zuri ndiyo dawa, wasiwasi huondoa,
Furaha moyoni huwa, hofu yako kuitoa,
Faraja wewe kupewa, na raha isiyo poa,
Neno zuri.

Ni hedaya neno zuri, muhimu kwayo dunia,
Upatapo ni fahari, moyo wako hutulia,
Haliyo iwapo shwari, mamboyo wajifanyia,
Neno zuri.

Neno zuri ni muhimu, kila mtu ahitaji,
Kulipata kuna hamu, neno zuri hufariji,
Neno zuri kweli tamu, hulifaidi mlaji,
Neno zuri.

3 comments:

 1. Nanukuu "Neno zuri ni muhimu, kila mtu ahitaji,
  Kulipata kuna hamu, neno zuri hufariji,
  Neno zuri kweli tamu, hulifaidi mlaji,
  Neno zuri." mwisho wa kunukuu:- Ni kweli kabisa mtani hakuna asiyependa kuambiwa maneno/neno zuri. Ahsante Mtani: Upendo Daima

  ReplyDelete
 2. Wasiwasi kitu kizuri
  Hutupa cha Kufikiri
  Hufanya tukajitokeza mafichoni
  Kutazama mambo ya moyoni
  Huweka ukweli wa dunia mbele
  Kwa wote hata wasio na kipaumbele

  Neno zuri kila siku
  Siri ya kulala vizuri usiku!

  ReplyDelete
 3. @Da Yasinta, ni kweli usemayo. Nimekaa nikafikiri kuna nyakati nikiwa na wasiwasi wowote na mtu akanipa neno la kunifariji, hunipa nguvu kubwa. Ndiyo maana naamini neno zuri ni dawa ya wasiwasi.

  @ Serina nawe umesema,
  Neno lenye hekima,
  Ila wasi ukikuandama,
  Na moyo kuuchoma,
  Neno zuri ni dawa njema.

  ReplyDelete