Monday, February 15, 2010

Pendo langu kwako wewe

Uketi chini mpenzi, ya moyoni nikwambie,
Daima nitakuenzi, uhai uniishie,
Hutoipata simanzi, nataka ufurahie,
Pendo langu kwako wewe, halipimwi kwa mizani.

Halipimwi kwa mizani, uzitowe wazidia,
Pendo linayo thamani, hakuna cha kufikia,
Hata kwa mizani gani, huwezi kulipimia,
Pendo langu kwako wewe, hutolikuta dukani.

Hutolikuta dukani, ati labda lauzwa,
Pendo li ndani moyoni, kwalo pendo nimemezwa,
Kwani halina kifani, kwa kitu likaigizwa,
Pendo langu kwako wewe, kwa mwingine hulikuti.

Kwa mwingine hulikuti, pendo akakupatia,
Nina pendo lenye dhati, ya moyo uloridhia,
Pendo liso na wakati, daima kufurahia,
Pendo langu kwako wewe, ling'aalo kama nyota.

Ling'aalo kama nyota, maishani kuwa nuru,
Pendo raha kulipata, kufaidi kwa uhuru,
Pendo chozi kunifuta, kwa nini nisishukuru,
Pendo langu kwako wewe, liishi zote dawamu.

Liishi zote dawamu, linipe raha ya moyo,
Pendo hili na lidumu, kwa furaha linipayo,
Pendo hili mbona tamu, kwa tamu niipatayo,
Pendo langu kwako wewe, kamwe halina mipaka.

Kamwe halina mipaka, pendo mali yako yote,
Kukupenda sitochoka, pendo ulimi na mate,
Juwa kwangu umefika, wala us'ende kokote,
Pendo langu kwako wewe, waache waone wivu.

Waache waone wivu, kwa pendo ninalokupa,
Sisi tule zetu mbivu, pendo lizidi nenepa,
Kwako niwe msikivu, sitowaza kukutupa,
Pendo langu kwako wewe, wacha lizidi shamiri.

Wacha lizidi shamiri, wacha pendo na ling'ae,
Kukupata ni fahari, wengine uwakatae,
Pendo kwako li mahiri, unifae nikufae,
Pendo langu kwako wewe, mbona linanipa raha.

Mbona linanipa raha, ni bahati sana mie,
Pendo lajaa furaha, wacha nilifurahie,
Kwa pendo nipate siha, nishibe na nichanue,
Pendo langu kwako wewe, ni mwisho wa mambo yote.

8 comments:

 1. nanukuu "Hutolikuta dukani, ati labda lauzwa,
  Pendo li ndani moyoni, kwalo pendo nimemezwa,
  Kwani halina kifani, kwa kitu likaigizwa,
  Pendo langu kwako wewe, kwa mwingine hulikuti." mwisho wa kunukuu;- hapa nimepapenda:-)

  Shairi la leo ningekuwa mimi ndo mpenzi wako mtani ningekujibu hivi Nimeketi chini mpenzi wangu na pia nakusikiliza utakalo kusema maana lina utamu kweli. Upendo daima

  ReplyDelete
 2. Papa Fadhy: shairi mwanana. naungana na Da Yasinta!

  laiti watu wote wangekuwa na 'wishes' kama hizo dunia leo ingekuwa pahala bora pa kuishi tofauti na sasa!

  Inashangaza kusikia wengine wakisema 'upendo wa Mume/nke wangu kwangu umekwisha/umepungua' kana kwamba unachotwa dukani ama mtoni :-(

  ReplyDelete
 3. Sijui kwanini nimejikuta naliimba kwa sauti!:-)

  Ushawahi kusoma kitu kimya kimya lakini unajijua mpaka kisauti ungeliimbaje?

  ReplyDelete
 4. Sijui kwanini nimejikuta naliimba kwa sauti!:-)

  Ushawahi kusoma kitu kimya kimya lakini unajijua mpaka kisauti ungeliimbaje?

  ReplyDelete
 5. Hahahahaaa Kitururu.
  Nimependa aliyefikiria ustaarabu wa kuweka kibofyo cha maoni chini.
  Maana nilijikuta nikiimba badala ya kusoma na kilichonifanya nitambue hilo ni Mama P kutodhani nimekuwa malenga mwema (japo najua alinogewa a maneno)
  Kaka Fadhy asante saana mkuu
  Hii imesimama
  Blessings

  ReplyDelete
 6. nawashukuruni nyote. Nimefurahi kuona shairi hili limewavutia. Nawashukuruni sana kwa kutonichoka na mashairi yangu. Pamoja daima!

  ReplyDelete
 7. shairi hili ama kwa hakika lina utamu wake na ujumbe wake ni wa kunata...

  ReplyDelete