Sunday, February 28, 2010

Moyo wangu tulia

Dunia ina vikwazo, we' moyo wangu tulia,
Ina mengi machukizo, yanoleta kuumia,
Ina mengi matatizo, mlo kujitafutia,
We' moyo wangu tulia, mtumainie Mola.

Maisha ni mapambano, moyo hilo walijua,
Hivyo ni mtafutano, wapaswa kulitambua,
Huwepo mivurugano, ni vema kuigundua,
We' moyo wangu tulia, mtumainie Mola.

Maisha ni kama vita, yapasa uwe na nia,
Moyo wala 'sije tweta, tamaa kujikatia,
Moyo zidi furukuta, malengo kuyafikia,
We' moyo wangu tulia, mtumainie Mola.

Moyo kuna wanadamu, mabaya hukuombea,
Chuki kwako iwe sumu, baya sije watendea,
Ila sala ni muhimu, kwa yote yanotokea,
We' moyo wangu tulia, mtumainie Mola.

Moyo uwe nayo nguvu, mwiko kukata tamaa,
Uwe na uvumilivu, hata ushinde na njaa,
Pia uwe msikivu, na kumaizi hadaa,
We' moyo wangu tulia, mtumainie Mola.

Mola wetu husikia, zidi mtumainia,
Moyo uzidi tulia, maisha wapigania,
Moyo utafurahia, lengo litapotimia,
We' moyo wangu tulia, mtumainie Mola.

1 comment:

  1. Ni kweli lazima kutulia na kumtumaini Mungu. Shairi huli la lao lina ujumbe mzuri pia huzuni. Natumaini mtani u salama.Jumapili njema.

    ReplyDelete